Vituo vya mafuta vinaishiwa bidhaa hiyo nchini Nigeria huku mkanganyiko ukitawala baada ya Rais aliyeapishwa Bola Tinubu kutangaza kufuta ruzuku kwa bidhaa za petroli.
Bei za pampu zimeongezeka zaidi ya mara tatu huku misururu mirefu ikishuhudiwa katika vituo vya mafuta katika miji mikubwa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kupanda kwa nauli ya usafiri.
Mkuu wa kampuni ya mafuta ya serikali ya NNPC mnamo Jumanne alihakikishia usambazaji wa kutosha wa mafuta nchini humo na kuwalaumu madereva kwa kununua "zaidi ya kile wanacho hitaji".
"Tunaelewa watu wataogopa mabadiliko yanayoweza kutokea ya bei ya petroli, lakini hiyo haitoshi kwa watu kukimbilia kwenye vituo vya mafuta kununua zaidi ya kile wanachohitaji. Tunaamini hali ya kawaida itaanza hivi karibuni," Mele Kyari alisema kwenye vyombo vya habari.
Timu ya Rais Tinubu ilieleza kuwa bajeti ya sasa haikutoa ruzuku ya mafuta zaidi ya Juni na kushutumu vyombo vya habari kwa "kukuza taarifa kwa upotofu".
"Serikali ya Tinubu imerithi tu utawala ambapo hakukuwa na kipengele cha ruzuku katika Sheria ya Ugawaji wa 2023 hadi Juni 2023," alisema Festus Keyamo, ambaye alikuwa msemaji wa kampeni ya urais.
Aliongeza kuwa rais "amekubali tu hali hii" katika hotuba yake ya kuapishwa.
Katika hotuba yake ya kuapishwa, Rais Tinubu alisema angeondoa ruzuku ya mafuta - iliyokadiriwa kugharimu karibu dola bilioni 10 mwaka jana. Ilikuwa ni moja ya ahadi zake za kampeni lakini juhudi za hapo awali za kumaliza zilisababisha maandamano ya ghasia.
Nigeria ni mzalishaji mkubwa wa mafuta barani Afrika lakini inategemea uingizaji wa bidhaa za petroli iliyosafishwa kwa matumizi ya ndani kwa sababu kwa miongo kadhaa, viwanda vyake vinne vya kusafisha mafuta havijafanya kazi ipasavyo.
Bilionea Aliko Dangote wiki iliyopita alifungua kiwanda cha kusafisha mafuta mjini Lagos - kikubwa zaidi barani Afrika - ambacho kimeelezwa kuwa kinaweza kubadilisha matatizo ya mafuta nchini Nigeria.