Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, amemsimamisha kazi gavana wa benki kuu ya nchi hiyo.
Katika taarifa yake siku ya Ijumaa, serikali ya Nigeria inasema kusimamishwa kazi kwa Godwin Emefiele, na rais Tinubu kunaanza ''mara moja''.
Inasema uamuzi huo ulikuwa dhidi ya hali ya nyuma ya ''uchunguzi unaoendelea'' katika shughuli za ofisi ya gavana wa benki kuu pamoja na mipango ya serikali kufanya ''mageuzi katika sekta ya fedha ya uchumi.''
Rais Tinubu ambaye aliapishwa mwishoni mwa mwezi uliopita, amemuagiza gavana aliyesimamishwa kazi ''kukabidhi mara moja shughuli za ofisi yake'' kwa naibu gavana anayesimamia oparesheni, Folashodun Adebisi, ''ambaye atakuwa mkuu wa oparesheni na gavana wa benki akisubiri kukamilika kwa uchunguzi na marekebisho.''
Serikali haijatoa maelezo kuhusu aina ya uchunguzi au masuala yanayohusika. Godwin Emefiele, 61, amekuwa gavana wa benki kuu ya Nigeria tangu 2014.
Nigeria ndiyo nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika. Benki Kuu ya Nigeria hivi karibuni imezua utata baada ya kuanza utekelezaji wa sera mpya ya sarafu.
Ilianzisha noti mpya zilizoundwa upya katika uchumi na kuondoa noti zilizopo katika kile ambacho mamlaka ilisema ni jaribio la kukabiliana na rushwa, kukabiliana na ukosefu wa usalama na kulazimisha fedha nyingi kurudi kwenye mfumo wa benki.
Benki hiyo ilisema zaidi ya 80% ya fedha katika mzunguko zilikuwa zikihifadhiwa na watu binafsi nje ya benki.
Sera iliyotekelezwa muda mfupi kabla ya uchaguzi wa rais wa Nigeria mwezi Februari ilisababisha uhaba wa fedha na foleni ndefu kwenye benki na mashine za kutolea fedha.
Hatua hiyo ilisitishwa baadaye na benki kuu kufuatia uamuzi wa mahakama kuu na malalamiko ya umma.