X kuanza kutoa huduma ya simu na video / Photo: AFP

Jukwaa la mtandao wa kijamii X litaanza kutoa huduma za video na sauti, mmiliki Elon Musk alitangaza Alhamisi akisema ni hatua ya kugeuza Twitter ya zamani kuwa "programu ya kila kitu."

"Huduma za video na sauti zinakuja kwa X," Musk aliandika katika chapisho kwenye jukwaa, bila kutaja ni lini huduma mpya zitapatikana.

Vipengele vya kupiga simu vitafanya kazi kwenye mifumo ya iOS, Android, Mac na PC, na hakuna nambari ya simu ingehitajika, alisema.

"X ni kitabu cha anwani cha kimataifa chenye ufanisi," bilionea huyo aliongeza, " hilo ni jambo la kipekee."

Kufanya Twitter upya

Mwezi uliopita, Musk na mtendaji mkuu wake mpya aliyeajiriwa Linda Yaccarino walitangaza kubadili jina la Twitter kuwa X, wakisema itakuwa "programu ya kila kitu".

Hii ilifuata mfumo wa WeChat ya China ambayo ingewaruhusu watumiaji kushirikiana na kuhifadhi hela zao.

Tovuti ya crypto CoinWire iliripoti kuwa tawi la X la malipo la Twitter Payments LLC lilipewa leseni "muhimu" ya kutuma fedha kutoka jimbo la Rhode Island nchini Marekani siku ya Jumatatu, na kuiruhusu "kujihusisha na shughuli zinazohusiana na sarafu ya cryptocurrency" kama vile kubadilishana fedha, pochi na kuchakata malipo.

Leseni inaruhusu X "kuhifadhi, kuhamisha, na kuwezesha ubadilishaji wa mali za kidijitali kwa niaba ya watumiaji wake," kulingana na CoinWire.

TRT Afrika