Na Ramadhan Kibuga
Nchini Burundi, Serikali imechukua uamuzi wa kupandisha bei ya mafuta ya magari. Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Wananchi wameshuhudia utekelezaji wa bei mpya katika vituo mbalimbali nchini humo ambapo hivi sasa lita moja ya mafuta itakuwa ni Franka 4450 sawa na dola 1,52.
Hata hivyo, kupanda kwa bei kunaonekana kuibua malalamiko miongoni mwa wananchi. Mussa Hakizimana ambae ni dereva wa taksi kwa zaidi ya miaka 8 mjini Bujumbura anasema tangu kuanza kwa bei mpya, hali ya maisha imekuwa ngumu.
"Mwanzo nilikuwa nafanya misafara mpaka 10, lakini leo kupata misafara 2,3 hadi 5 ni shida." Musa ameongeza kusema kuwa gari zinahitaji huduma nyingi ikiwemo kuosha, kufanyiwa matengenezo na bado kuna mapato ya barabarani hivyo kubakiwa na fedha kidogo mfukoni.
"Kwa kweli tuombe serikali ilitizame suala hili vizuri. Tuna vitu tunalipa serikalini, malipo ya nyaraka yamepanda. Tutajikuta mwisho wa siku tunashindwa hata kulipia ada za watoto, lakini pia tutashindwa kutunza gari zetu, mwisho wa siku tutakuwa hatuna kazi," amesema Musa.
Bei zimepanda wakati Burundi imeshuhudia katika siku za nyuma uhaba mkubwa wa mafuta kiasi cha kushuhudiwa kwa foleni ndefu za magari katika vituo vya mafuta.
Hali hii ya upandaji wa bei za mafuta au kukosekana kwa bidhaa hiyo imewaathiri pia wafanyabiashara.
Ally Omar ambae ni mfanyabiashara katikati ya mji wa Bujumbura anasema, "Tunahesabu hela ya usafiri pamoja na hela ya kulangua ndio tujue utaratibu wa kuuza bidhaa zetu. Lakini kila kukicha bei za mafuta zinapanda kiasi kwamba upande wetu hatujui ni kiasi gani tunaweza kuongeza kwenye bei zetu. Mara tunaongeza Franka elfu 2, elfu 5 au hata elfu 10 mpaka wateja wanahisi kwamba tunawaibia au kuwafanyia utapeli."
Kama Serikali tumejaaribu kuchukua hatua ili kukabiliana na mabadiliko hayo. Nia yetu ni kupunguza maumivu kwa raia. Ndio maana tumesamehe baadhi ya kodi.
Mfanyabiashara huyo licha ya kero hiyo hajakata tamaa. "Ni kupambana tu kwa vyovyote vile, bila kazi itakuwa vigumu kuishi,” huku akiiomba serikali kustawisha bei za mafuta na bidhaa nyengine muhimu.
Isitoshe bei za mafuta zimepanda sambamba na bei za nauli katika nchi nzima na hivyo kutatiza maisha ya raia. Lakini serikali imetetea uamuzi wake kwamba unatokana na soko la kimataifa na kwamba imefanya juhudi kubwa ya kupunguza maumivu kwa raia.
Ibrahim Uwizeye ni Waziri wa Burundi wa Nishati anasema, "Hatuzalishi mafuta ya magari hapa nchini Burundi. Na bei za mafuta zinapangwa katika soko la kimataifa. Kama Serikali tumejaaribu kuchukua hatua ili kukabiliana na mabadiliko hayo. Nia yetu ni kupunguza maumivu kwa raia. Ndio maana tumesamehe baadhi ya kodi. Na ukitizama bei zetu za mafuta ziko chini ukilinganisha na mataifa jirani."
Mbali na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kama vile sukari na vyakula, hivi sasa pia, bei ya mbolea imepanda nchini humo, ambapo asilimia 80 ya raia wake wanategemea shughuli za kilimo.