Ujumbe wa gari kwenye ua la hoteli hiyo./Picha: Wengine

Na Gaure Mdee

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Habari zilisambaa mtandaoni kuwa watalii wanne kutoka Israel wamelazimika kuihama hoteli baada ya kukerwa na ujumbe wenye kuiunga mkono Palestina na kulaani mauaji yanayofanywa na Israel katika eneo la Gaza.

Wageni hao walifika katika hoteli ya Canary Nungwi iliyoko visiwani humo, siku ya Aprili 18, 2024 kwa lengo la kupata huduma ya malazi.

Hata hivyo, wageni hao walioneshwa dhahiri kuchukizwa na ujumbe wa 'Free Palestine', uliokuwa umebandikwa kwenye gari la mmiliki wa hoteli hiyo.

Katika mahojiano yake na TRT Afrika, siku ya Ijumaa 19 Aprili, mmiliki wa hoteli hiyo, bwana Ali Mohamed, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa, wageni hao walitaka kuondolewa kwa gari hilo katika eneo hilo.

"Baada ya kufika tu, wageni hao walisema hawakufurahishwa na ujumbe uliokuwa kwenye gari hilo," anaeleza Mohamed, ambaye pia ni mmiliki wa gari hilo.

Muonekano wa mandhari ya kupendeza ya visiwa vya Zanzibar./Picha: Wengine

Kulingana na Mohamed, wageni hao hawakufurahishwa na hatua ya mmiliki wa hoteli hiyo kuiunga mkono Palestina.

"Niliwaaambia kuwa huwa ndio msimamo wangu, sikuwa tayari kuondoa gari kama hawakutaka kukaa hapo, walikuwa na uhuru wa kuhamia hoteli nyingine," anasema.

Mmiliki huyo wa hoteli ya Canary, amesisitiza haja ya Israel kusitisha mauaji ya kinyama katika eneo la Gaza, na kusema ni wakati muafaka Palestina inakuwa huru.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina katika eneo la Gaza yameingia siku ya 196, ambapo watu 34,012 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 76,833 wakiwa wamejeruhiwa.

TRT Afrika