Kimbunga Chido kimeua takriban watu 94 nchini Msumbiji kufikia Disemba 15, 2024. / Picha: Reuters

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, ( WFP) inasema kuwa Takriban watu milioni 3.3 hawana uwezo wa kuweka chakula mezani nchini Msumbiji.

Kati yao watu 770,000 wanakabiliwa na viwango vya dharura vya njaa.

"Mzozo wa kaskazini unatatiza maisha na kupunguza upatikanaji wa huduma za msingi kwa wakimbizi wa ndani na jamii za mitaa. Kuongezeka kwa ghasia katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado kumesababisha karibu watu 715,000 kuyahama makazi yao, " ripoti ya WFP imesema.

Mgogoro mkubwa zaidi wa usalama wa chakula unajitokeza katika maeneo ya kusini mwa Afrika, unaosababishwa na ukame wa mvua za El Niño.

Nchini Msumbiji kulingana na uchambuzi, katika msimu wa Oktoba 2024 hadi Machi 2025 karibu watu milioni 3.3 wanatarajiwa kuwa na uhaba wa chakula.

Madhara mabaya ya Kimbunga Chido, kilichopiga Cabo Delgado tarehe 15 Disemba 2024, kinaweza kuzidisha hali ya kibinadamu ya Msumbiji hata zaidi, huku takriban watu 680,000 wakiripotiwa wakiathiriwa na maafa hayo.

Kimbunga Chido kiliwauwa takriban watu 94 nchini humo.

TRT Afrika