Baadhi wa wakazi wa Kinshasa waliojitokeza mapema kupiga kura. Zaidi ya raia milioni 40 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanapiga kura nchini humo kuchagua viongozi wao. Picha/TRT Afrika. 

12:52 EAT

Denis Mukwege akiwa katika kituo chake cha kupigia kura mapema hii. Mukwege ni miongoni mwa wagombea urais nchini DRC.

Denis Mukwege, mgombea urais nchini DRC. Picha/TRT Afrika.

12:28 EAT

Mmoja wa waangalizi kutoka Zambia Enoch Kavindele, amewataka wananchi wa DRC kujitokeza kwa wingi na kupiga kura. “Nataka kusema kuwa, hii ndio nchi pekee waliyokuwa nayo, hivyo wajitokeze na wachague viongozi wao. Inaonekana watu wanashauku ya kutaka kupiga kura, hivyo tunawahimiza waje,” amesema Kavindele.

Enoch Kavindele, mwangalizi wa uchaguzi kutoka Zambia. Picha/TRT Afrika.

DRC imeruhusu waangalizi kutoka AU na SADC tu.

12:00 EAT

Martin Fayulu mmoja wa wagombea urais nchini DRC, punde tu baada ya kupiga kura, aliongea na waandishi wa habari na kusema, ‘’Kwa taarifa nilizopata kutoka majimboni ni kuwa kuna baadhi ya vituo hapa Kinshasa bado havijafunguliwa, na vilivyofunguliwa havina vifaa na vitendea kazi kamilifu kama mashine za kieletroniki. Lakini kiujumla zoezi linakwenda vyema na salama nawataka wananchi waende vituoni wakapige kura.’'

Martin Fayulu, muda mfupi baada ya kupiga kura. Picha/TRT Afrika. 

09:15 EAT

Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya taifa la DRC mapema leo, wamejitokeza kuchagua viongozi wao kuanzia ngazi ya urais, ubunge na madiwani.

Kuna jumla ya wagombea urais 26, huku rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi akiwania muhula wa pili. Katika uchaguzi huu, Tshisekedi anatoana jasho na wapinzani wake wakuu ambao ni Martin Fayulu, aliyekuwa waziri mkuu wa zamani.

Baadhi ya wapiga kura wakisubiri katika foleni. Picha/TRT Afrika. 

Vile vile mmiliki wa TP Mazembe, klabu kongwe ya mpira wa miguu maarufu na yenye mafanikio makubwa kwenye historia ya soka nchini DRC na Afrika kwa ujumla, Moise Katumbi anategemea kutumia uzoefu wake wa uongozi kama Gavana wa Katanga.

Katika majimbo 26, yatakayopigiwa kura, Kinshasa ndio inaongoza kwa idadi kubwa ya wapiga kura ambao wanafikia 5, 062, 991. Huku wastani wa majimbo mengine ukibaki kuwa ni wapiga kura milioni 1.3 kwa kila jimbo.

Kwa mara nyengine, uchaguzi wa mwaka huu pia umevutia mgombea mwanamke katika nafasi ya urais.

Marie Josee Ifoku (58) maarufu, ‘‘Mama wa fagio’’ hii ni mara yake ya pili kushiriki uchaguzi kama mgombea wa urais. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2018. Ifoku anaweka wazi uwezo wake na tajiriba aliyoipata mwaka 2018 kuwa imemfunza na itamsaidia kushinda mwaka huu.

Wakati huo huo, DRC imetangaza kufunga mipaka yake siku ya uchaguzi. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu DGM, ndege za ndani zimesitishwa, isipokuwa ndege za kimataifa katika viwanja vya ndege vya kimataifa.

TRT Afrika