(FILES) Profesa Jean-Jacques Muyembe-Tamfum alichangia kwa ugunduzi wa chanjo ya virusi vya ebola aina ya Zaïre  / Photo: AFP

Shirika la Afya duniani WHO, limempa profesa Jean-Jacques Muyembe-Tamfum tuzo la viongozi wa afya duniani.

Hili ni tuzo la mafanikio ambayo hutolewa na mkurugenzi mkuu wa shirika la WHO kwa watu walichangia vikubwa katika sekta ya afya .

Profesa Jean-Jacques Muyembe-Tamfum ametunikiwa kwa ubunifu, uongozi na michango yake ya msingi katika usimamizi na matibabu ya magonjwa kama vile Ebola.

"Amefanya kazi bila kuchoka kujenga uwezo wa kisayansi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuanzisha vituo vingi vya utafiti nchini humo, na amecheza majukumu muhimu na shirika la afya duniani WHO katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza," shirika la WHO limesema katika taarifa.

Je, Profesa Muyembe-Tamfum ni nani?

Profesa Jean-Jacques Muyembe-Tamfum alizaliwa mwaka wa 1942 na ni mwananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Yeye ni daktari , na kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya kitaifa ya utafiti wa tiba ya kibiolojia ya DRC.

Profesa Muyembe-Tamfum alikuwa kati ya timu ya wataalamu iliyogundua virusi vya Ebola aina ya Zaïre wakati wa mlipuko wa kwanza uliorekodiwa mwaka 1976, katika mkoa wa Equator, nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.

Baadaye alisaidia kubuni mojawapo ya matibabu ya kwanza ya ufanisi dhidi ya virusi na kupelekwa kwa chanjo ya majaribio ya ugonjwa wa Ebola.

Ugonjwa wa virusi vya Ebola ni ugonjwa nadra lakini hatari kwa wanadamu. Inapatikana kwa kuhusiana moja kwa moja na mtu aliyeambukizwa. Pia inaweza kuambukizwa kwa kula wanyama walioambukizwa na virusi hivyo.

Kuna chanjo madhubuti ya Ebola aina ya Zaire , ambayo hupatikana zaidi Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tangu mwaka 1976 , DRC imekumbwa na mlipuko wa ebola mara 14 , hasa virusi aina ya Zaire.

WHO inasema utafiti unaendelea ili kupata chanjo na matibabu ya aina nyingine tano ya Ebola.

Shirika la afya duniani pia linamtambua Profesa Muyembe-Tamfum kwa kujenga uwezo wa kisayansi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuanzisha vituo vingi vya utafiti nchini humo, na kusaidia WHO kupambana na magonjwa ya kuambukiza.

Profesa Muyembe-Tamfum amepokea angalau tuzo 10 za kimataifa kwa mchango wake katika sekta ya afya nchini DRC, barani Afrika na kimataifa.