Wakimbizi wa kiislamu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wapata shida kupata chakula wakati wa Ramadhani.
Mamia ya Waislamu nchini DRC washiriki mwezi tukufu wa Ramadhani na wanatarajia kuomba amani irejee nchini humo.
Waislamu kama Issa Bendelo, ambaye alikimbia kijiji chake anafunga kwa ajili ya amani. "Katika mwezi huu wa Ramadhani, nitaomba amani irudi nyumbani." Anasema Bendelo.
Bendelo anawapa futari na maji baadhi ya Waislamu waliokimbia makazi yao.
Kwake yeye, hii ni mara yake ya kwanza kushiriki mwezi mtukufu wa Ramadhani ndani ya kambi ya wakimbizi baada ya waasi wa M23 kushambulia kijiji chake cha Rumangabo na kuua wanafamilia wengi.
"Natumai kuwa Mwenyezi Mungu atajibu maombi yetu na amani itarejea nchini Kongo," anaongeza Issa Bendelo.
Wakati wa mwezi wa Ramadhani, Waislamu hula pamoja na kushiriki chakula na maskini baada ya kufunga siku nzima.
DRC ina Waislamu takribani milioni tano sawa na asilimia 3 ya wakazi wote. Uislamu ni dini ya pili kwa ukubwa nchini baada ya Ukristo.
DRC ni miongoni mwa nchi tajiri zaidi katika bara la Afrika, lakini utajiri wake ni miongoni mwa vyanzo vya migogoro mikubwa nchini.
Misaada ya kibinadamu
Kulingana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa, UN, waasi wa Uganda wa ADF ni wanamgambo wenye silaha ambao wana mahusiano na kundi la DAESH jambo ambalo limewaweka watu kama Hadji Mousa Kalombo kwenye wasiwasi.
“Natoa wito kwa Waislamu wote duniani kuja kuwasaidia Waislamu wanaopigana nchini Kongo ili waweze kupata futari,” anasema Hadji Moussa Kalombo wakati wa mahojiano na TRT Afrika.
Waislamu wengi hapa Kongo watashiriki Ramadhani tukufu bila familia zao katika hali na mazingira magumu - Mwenyezi Mungu aturehemu, mioyo yetu iwaendee… Hili lazima liishe. Uislamu ni dini ya amani” anaongeza Kalombo.
Ramadhani hii ni ya kipekee kwa sababu Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina wasiwasi mkubwa kwamba miezi kadhaa ya vurugu na ukosefu wa usalama katika majimbo ya mashariki ya Ituri na Kivu Kaskazini imewaweka mamilioni ya watu katika matatizo.
Sasa kuna wakimbizi wa ndani milioni 6.2 nchini DRC, asilimia 65 kati yao wako Ituri na Kivu Kaskazini.
Kutokana na vurugu hizo, uhaba wa chakula unaongezeka katika nchi yenye zaidi ya watu milioni 26.4 wakihangaika kupata chakula cha kutosha kila siku; utapiamlo na magonjwa ya mlipuko kama vile surua na kipindupindu yanaongezeka, na hivyo kupunguza uwezo wa jumuiya ya binadamu na asasi za kiraia kujibu.
Katika tukio nyingine kama hii, wiki iliyopita AP iliripoti juu ya wakimbizi wa ndani wa Kisomali wanaofuturu kwa maji pekee wakati nchi inakumbana na ukame mrefu zaidi iliyowahi kurekodiwa nchini.