Shirika la afya Duniani, WHO limesema kuwa zaidi ya vifaa 1.2 milioni vya vipimo vya haraka vya maradhi ya kipindupindu vitasambazwa katika nchi 14, huku shehena ya kwanza ikitarajiwa kuwasili nchini Malawi, siku ya Ijumaa.
WHO limesema usambazaji rasmi wa vifaa vya kupimia kipindupindu kupitia shirika la Gavi the Vaccine Alliance, utaboresha ugunduzi na ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko kwa wakati unaofaa, ufanisi wa kampeni za chanjo katika kukabiliana na milipuko ya sasa, na kulenga juhudi za baadaye za chanjo.
“Ni janga kuona kipindupindu—ugonjwa unaozuilika na unaotibika—unaendelea kutesa na hadi kuua leo. Tunahitaji hatua za haraka katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja kwa nchi kuonesha uwajibikaji katika kutoa huduma za maji safi, na usafi wa mazingira," alisema Dkt. Michael Ryan, Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Dharura wa Afya wa WHO.
Nchi ambazo zinategemewa kupokea shehena kubwa zaidi kupata kutokea ulimwenguni ni pamoja na zile zilizoathiriwa sana na milipuko ya kipindupindu, kama vile Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Sierra Leone, Somalia, Uganda, Zambia, na Zimbabwe.
" Mpango huu utaboresha uwezo na usahihi wa kutambua na kukabiliana na milipuko kwa kuongeza uwezo wa ufuatiliaji na upimaji wa kawaida na kusaidia kutambua kwa haraka visa vya kipindupindu vinavyoweza kutokea," shirika la WHO limesema.
Takwimu za WHO zinaonesha kuwa hadi kufikia Machi 3, 2024 kesi 335 059 za kipindipindu zilikuwa zimeripotiwa na vifo 6197, huku asilimia 70 ya visa hivyo vikiripotiwa katika Jamhuri Ya kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Malawi, Msumbiji na Nigeria.
Kimsingi, itasaidia pia nchi kufuatilia mienendo na kujenga msingi wa ushahidi kwa ajili ya programu za kinga za siku zijazo, kusaidia kufikiwa kwa shabaha za udhibiti wa kipindupindu za kitaifa na kutokomeza.
"Uchunguzi wa haraka utasaidia kubainisha maeneo yanayovutia zaidi kwa usahihi mkubwa. Hii inaruhusu watoa huduma kulenga chanjo ya kipindupindu kwa wakati muafaka na mahali sahihi ili kuokoa maisha zaidi ," Leila Pakkala, Mkurugenzi wa idara ya usambazaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa la watoto, UNICEF.
Shirika la WHO linasema kuwa visa vya kipindupindu vimekuwa vikiongezeka duniani toka mwaka 2021, huku kukiwa na viwango vya juu vya vifo licha ya kuwepo kwa matibabu na ufanisi mkubwa.
WHO inasema idadi kubwa ya milipuko imesababisha mahitaji ya chanjo ambayo hayajawahi kufanywa kutoka kwa nchi zilizoathiriwa.