Shirika la afya Duniani, WHO linasema kuongezeka kwa vurugu za hivi majuzi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumesababisha vifo vingi vya watu, kiwewe, kuhama makazi, na uharibifu wa miundombinu muhimu ya afya, na kuzidisha hali ambayo tayari ni mbaya kwa mamilioni ya watu.
" Hali inabaki kuwa ya wasiwasi na tete, na mahitaji ya afya ni makubwa. WHO imebaki nchini humo na imeendelea kujitahidi kutoa huduma za afya kwa kutoa vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha, kusaidia wahudumu wa afya, na kuratibu huduma za dharura," WHO imesema katika taarifa.
WHO inasema watu wanaohitaji huduma za hospitali ni wengi na vyumba vya kuhifadhi maiti vimejaa kupita kiasi.
" Tangu tarehe 26 Januari, 3082 waliojeruhiwa na 843 wamekufa wameripotiwa kutoka vituo 31 vya afya ndani na karibu na Goma, Kivu Kaskazini. Pamoja na kuendelea kwa ghasia zaidi kusini, majeruhi 65 waliripotiwa kutoka hospitali 3 za Kivu Kusini," WHO imesema.
" Kuona miili ikiwa imelala bila kuhifadhiwa inatisha. Ingawa miili ya watu waliokufa kutokana na jeraha kwa ujumla haiwezi kueneza magonjwa, ni haki ya wafu kutambuliwa na kuzikwa kwa utaratibu unaofaa," WHO imeongeza.
Zaidi ya 70 (au 6%) ya vituo vya afya katika Kivu Kaskazini vimeathirika, na vingine kuharibiwa kabisa na vingine vikijitahidi kuanzisha upya shughuli zao.
Baadhi ya magari ya kubeba wagonjwa pia yameharibika. Kliniki ya afya inayopata msaada wake kutoka kwa WHO huko Kivu Kaskazini ilikaliwa kwa muda na makundi yenye silaha.
Wahudumu wa afya wamelazimika kukimbilia usalama, huku katika maeneo mengine, wamekuwa wakifanya kazi usiku kucha, wakiwa na uwezo mdogo wa kukabiliana na mahitaji mengi, na wakati mwingine maisha yao wenyewe yakiwa hatarini.