Shirika la Afya Duniani (WHO) limependekeza chanjo ya pili ya malaria kwa watoto.
Shirika hilo la afya linasema chanjo ya R21/Matrix-M iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza na kutengenezwa na Taasisi ya Serum ya India, tayari imeidhinishwa kutumika nchini Burkina Faso, Ghana na Nigeria.
Malaria inaua zaidi ya watu 600,000 kila mwaka duniani kote, wengi wao wakiwa watoto barani Afrika.
"Kama mtafiti wa Malaria, nilikuwa na ndoto kuwa siku moja tutakuwa na chanjo salama na yenye ufanisi dhidi ya malaria. Sasa tuna mbili," mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema wakati wa mkutano huko Geneva Jumatatu.
Haja ya chanjo ya pili
Chanjo ya RTS,S, iliyotolewa na kampuni kubwa ya dawa ya Uingereza GSK, imekuwa ya kwanza kupendekezwa na WHO mwaka 2021 ili kuzuia malaria kwa watoto katika maeneo yenye maambukizi ya wastani hadi ya juu ya malaria.
"GSK daima imetambua haja ya chanjo ya pili ya malaria, lakini inazidi kudhihirika kuwa RTS,S, chanjo ya kwanza kabisa ya malaria na chanjo ya kwanza kabisa dhidi ya vimelea kwa binadamu, iliweka kigezo kikubwa," GSK ilisema katika taarifa.
Kampuni hiyo iliongeza kuwa zaidi ya watoto milioni 1.7 nchini Ghana, Kenya na Malawi wamepata angalau dozi moja ya chanjo hiyo , na itasambazwa katika mataifa mengine tisa yenye malaria kuanzia mapema mwaka ujao.
WHO ilisema chanjo zote mbili zimeonyesha ufanisi sawa katika majaribio tofauti, lakini bila majaribio ya ana kwa ana hakuna ushahidi unaoonyesha kama moja ilifanya vyema zaidi.
Shirika hilo limeziachia nchi kuamua ni bidhaa gani zitatumia kwa kuzingatia mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kumudu bei na usambazaji.
Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti, alisema chanjo hiyo mpya ina uwezo mkubwa kwa bara hilo kwa kusaidia kuziba pengo kubwa la mahitaji na usambazaji.
"Zikitolewa kwa kiwango kikubwa na kusambazwa kwa upana, chanjo hizo mbili zinaweza kusaidia kuimarisha juhudi za kuzuia na kudhibiti malaria na kuokoa mamia ya maelfu ya maisha ya vijana barani Afrika kutokana na ugonjwa huu hatari," alisema Dkt Moeti.