Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa zaidi ya wakimbizi 200,000 nchini Tanzania watapokea nusu ya mgawo wa chakula kuanzia mwezi ujao kutokana na ukosefu wa ufadhili kutoka kwa wafadhili.
Ugawaji wa chakula kwa wakimbizi nchini Tanzania - ambapo asilimia 70 ni kutoka Burundi na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - umepunguzwa taratibu tangu mwaka 2020, WFP ilisema katika taarifa yake Jumanne.
Hatua za kupunguza mgawo wa chakula, ambazo ni za pili nchini Tanzania katika miezi ya hivi karibuni, zinakuja baada ya hatua kama hizo kuchukuliwa sehemu mbalimbali duniani huku shirika la chakula la Umoja wa Mataifa likikabiliwa na upungufu wa fedha na bei kubwa ya chakula, hali ambayo inatokana na mzozo nchini Ukraine.
Mwezi Machi, mgao huo, ambao ulilenga kukidhi kiwango cha chini kilichopendekezwa cha kalori 2,100 kwa mtu kwa siku, ulishushwa kutoka asilimia 80 ya kiwango hicho hadi asilimia 65. "Mwezi Juni, mgawo utapunguzwa zaidi hadi asilimia 50, ambayo inaweza kuwaacha maelfu ya wakimbizi wakipambana kukidhi mahitaji yao ya lishe," WFP ilisema, ikiongeza kuwa inahitaji dharura dola milioni 21 ili kuepuka kupunguza zaidi.
Mkurugenzi wa nchi wa shirika hilo Tanzania, Sarah Gordon-Gibson, alisema: "WFP ina wasiwasi mkubwa kuwa kupunguzwa kwa kiasi hicho kutawalazimisha wakimbizi kuwa katika hatari zaidi." WFP ilitangaza mwezi Machi kuwa mgao wa chakula utapunguzwa pia kwa wakimbizi nchini Burundi na Bangladesh, na iliomba ufadhili wa dharura ili kuepuka kupunguza zaidi nchini Yemen.
Pia imepunguza mgawo wa chakula katika sehemu zingine za Afrika Mashariki katika miaka ya hivi karibuni kutokana na masuala ya ufadhili, ikiwemo katika sehemu zilizoathiriwa na maafa nchini Ethiopia, Sudan Kusini, na Kenya.