Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale amemtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua kuongoza vita dhidi ya Muguka huku kaunti tatu za Pwani ya Kenya zimepiga marufuku ya kuuza au kutumia mmea huo.
Akizungumza katika eneo la Eastleigh jijini Nairobi wakati wa ufunguzi wa kituo cha biashara, Duale alibainisha kuwa Gachagua amefanya vizuri katika vita vyake dhidi ya unywaji wa pombe haramu na mihadarati, hivyo basi mchango wake unahitajika katika kudhibiti utumiaje wa muguka.
“Ikiwa tunapigana na pombe katika eneo la kati ya Kenya, Bonde la Ufa na kila sehemu ya Kenya lazima pia tupigane na muguka,” alisema Duale.
"Nitamuomba Naibu Rais katika muda wa wiki mbili zijazo kuitisha mkutano huo kwa sababu yeye ni Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya na tutajadili kwa uwazi madhara ya Muguka kwa baadhi ya mikoa na jamii."
Kaunti ya Mombasa ilikuwa kaunti ya kwanza kutangaza marufuku hio, huku Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir, akiangazia kuwa utumiaji wa muguka umeharibu vijana na hata watoto wanaokwenda shule.
Gavana huyo pia alisema katika mahojiano ya Citizen TV, "Asilimia 30 ya wanaotumia muguka ni watoto chini ya miaka 18."
Na pia kusisitiza ya kwamba mieizi miwili baada ya kuapishwa kama Gavana wa Mombasa aliwasiliana na wafanyabiashara wa muguka kuliangalia vile wanaweza kulishughulikia suala hilo lakini bado wanaendela kuuzia watoto wadogo na inapatikana kwa bei rahisi sana.
Kuwajibu viongozi wanaokejeli hatua ya kupiga marufuku muguka, amesema "Hatuwezi kuharibu jamii, maisha ya watoto na usalama wetu kwa sababu muguka ni kitenga uchumi cha baadhi ya watu."
Kaunti ya Kilifi na Taita Taveta pia zilifuata mkondo huo na kupiga marufuku uingizaji, utumiaji, na uuzaji wa Muguka katika kaunti zao.
Kaunti ya Kwale hadi sasa haijapiga marufuku, lakini imependekeza kwenye mswada wa fedha 2024, kwamba wale watakaoendelea kufanya biashara ya bidhaa hiyo sasa watalazimika kulipia kibali cha shilingi elfu 50,000, na sio elfu 10 kama ilivyokua hapo awali.
Vilevile kaunti tatu za kaskazini mashariki mwa Kenya, Wajir, Garissa, na Mandera zinatarajiwa kuungana na kaunti za pwani katika kuweka marufuku ya mmea huo.