Guillaume Soro aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Côte d'Ivoire kati ya 2007 na 2012. / Picha: AFP

WAZIRI Mkuu wa zamani wa Côte d'Ivoire Guillaume Soro, aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kudhoofisha usalama wa taifa, amesema ameamua kukomesha uhamisho wake wa kujitakia ulioanza mwaka 2019.

"Ninatangaza hapa na sasa ninakomesha uhamisho wangu kwa sababu ni vigumu kwangu kuishi mbali na ardhi ya babu zangu na asili yangu ya Afrika," Soro alisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii Jumapili.

Mnamo Juni 2021, mahakama nchini Côte d'Ivoire ilimhukumu Soro kifungo cha maisha bila kuwepo mahakamani kwa tuhuma za kupanga mapinduzi dhidi ya Rais Alassane Ouattara mwishoni mwa 2019.

Soro, ambaye amekuwa uhamishoni barani Ulaya, alishtakiwa kwa kula njama na jaribio la kushambulia mamlaka ya serikali.

Kiongozi huyo wa zamani wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 51 aliwahi kuwa waziri mkuu wa Côte d'Ivoire kati ya 2007 na 2012. Pia aliwahi kuwa spika wa bunge.

TRT Afrika