Wahudumu wa afya nchini Ivory Coast walianza kuwapa watoto chanjo ya hivi punde zaidi ya ugonjwa wa malaria siku ya Jumatatu, mwanzo wa kampeni ya kikanda ambayo wataalam wanatumai inaweza kupunguza athari za mojawapo ya maradhi yanayo sababisha vifo vingi zaidi barani Afrika.
Ivory Coast imekuwa ya kwanza kuanza kusambaza chanjo hiyo ikilenga watoto wapatao 250,000 walio chini ya miaka miwili.
Chanjo hiyo ya dozi tatu inayojulikana kama R21/Matrix-M ilitengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza na iliidhinishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni Oktoba mwaka jana.
Utafiti unaonyesha kuwa ina ufanisi zaidi ya 75% katika kuzuia magonjwa na vifo vikali katika mwaka wa kwanza na kwamba kinga huongezwa kwa angalau mwaka mmoja zaidi kwa kupata chanjo ya ziada yaani booster.
Hii ni chanjo ya pili ya aina yake kutolewa na WHO. Mnamo 2021, WHO iliidhinisha chanjo ya kwanza ya malaria, inayojulikana kama Mosquirix, au (RTS,S) iliyotengenezwa na GSK.
Lakini chanjo hiyo inahitaji dozi nne na kinga yake hufifia ndani ya miezi kadhaa.
GSK pia hapo awali ilisema itaweza kutengeneza takriban dozi milioni 15 pekee.
Lakini Taasisi ya Serum ya India inayotengeneza hii chanjo mpya ya Oxford inayotumiwa Ivory Coast, tayari imetengeneza dozi milioni 25 za chanjo na inasema inapanga kutengeneza angalau milioni 100 kila mwaka, kwa bei nafuu ya takriban $4 kwa kila dozi.
Baadhi ya nchi 15 za Afrika zinapanga kuanzisha moja ya chanjo mbili za malaria mwaka huu kwa msaada kutoka kwa muungano wa kimataifa wa chanjo ya Gavi.
Chanjo hiyo inakusudiwa kufanya kazi pamoja na juhudi zingine za kuzuiamaambukizi - kama vile kulala chini ya Vyandarua - , kupuliza dawa y akuua mbu, kuzuia maji taka inayokaa karibu nanyumba na nyinginezo.
Zaidi ya 94% ya takribani visa milioni 249 vya malaria duniani na vifo 608,000 kila mwaka hutokea barani Afrika. Ugonjwa huo wa vimelea huenezwa na mbu na mara nyingi huwapata watoto chini ya miaka mitano na mama wajawazito.