Chanjo ya malaria ya R21 inatengenezwa na Taasisi ya Serum ya India, Pune / Picha: Reuters

Côte d'Ivoire wiki hii ilipokea chanjo yake ya kwanza dhidi ya malaria, ugonjwa ambao unaua watu wanne kwa siku nchini humo, wengi wao wakiwa watoto wadogo, serikali ilisema Jumamosi.

Jumla ya dozi 656,600 zimepokelewa, ambazo "hapo awali zitachanja watoto 250,000 wenye umri wa kati ya miezi 0 na 23" katika mikoa 16, serikali ilisema.

Ingawa idadi ya vifo vinavyotokana na malaria vimepungua kutoka 3,222 mwaka 2017 hadi 1,316 mwaka 2020 nchini Côte d'Ivoire, ugonjwa huo "unasalia kuwa sababu kuu ya mashauriano ya matibabu", kulingana na Wizara ya Afya.

Chanjo ya R21/Matrix-M imeidhinishwa na Ghana, Nigeria, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Serikali ya Ivory Coast pia inasambaza vyandarua na inanyunyizia dawa katika maeneo ambayo yamekithiri.

Malaria husababisha homa, maumivu ya kichwa na baridi, na inaweza kuwa mbaya au hata kuua ikiwa haitatibiwa.

Mwaka 2022, ilisababisha vifo zaidi ya 600,000 duniani kote, asilimia 95 kati yao wakiwa barani Afrika, na asilimia 80 kati yao katika watoto walio chini ya umri wa miaka 5, kulingana na WHO.

Chanjo hiyo ni chanjo ya pili ya malaria ambayo Shirika la Afya Duniani (WHO) limependekeza kwa watoto na inatengenezwa na Taasisi ya Serum ya India (SII).

TRT Afrika