Waziri wa mawasiliano wa Congo Thierry Moungalla amekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba kulikuwa na jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Denis Sassou Nguesso siku ya Jumapili.
Moungalla alitumia ukurasa wake wa X Jumapili jioni na kusema ilikuwa "ni dharura" kukanusha "habari hizo bandia."
“Habari za uongo zinaashiria matukio mazito yanayoendelea Brazzaville. Serikali inakanusha habari hizi za uongo, "alisema kwenye X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter.
"Tunawahakikishia umma juu ya utulivu unaotawala (nchini Congo), na tunawaalika watu waendelee na shughuli zao kwa utulivu."
Ripoti, ambazo chanzo chake bado hakijafahamika, zilisambaa kwa mara ya kwanza kwenye X na Telegram zikidai kuwa kulikuwa na "jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini Congo Brazzaville."
Rais Nguesso aliwasili New York, Marekani siku ya Jumapili kwa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Rais Nguesso mwenye umri wa miaka 79 amehudumu kama rais wa nchi hiyo ya Congo Brazaville kwa jumla ya miaka 38 - miaka 25 kutoka Oktoba 1997 hadi sasa, na miaka 13 kati ya 1979 na 1992.