Waziri Selemani Jafo akijumuika na wananchi katika kuadhimisha siku ya Usafi Duniani | Picha: Wizara ya Mazingira Tanzania

Na Ronald Sonyo

Siku ya usafi Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuiepushia dunia matatizo yanayosababishwa na uchafu unaozalishwa na watu.

Siku hii pia hutumiwa na viongozi wa serikali kuelekeza jamii umuhimu wa kuzingatia usafi kwa afya. Hata hivyo, mara kadhaa maelekezo hayo hushindwa kutekelezwa kutokana na uhaba wa miundombinu rafiki.

Mji wa Dodoma nchini Tanzania, ni miongoni mwa miji inayokuwa kwa kasi kwa kushuhudia ongezeko la idadi kubwa ya watu unao ambatana na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Baadhi ya wakazi wa jijini Dodoma wakiadhimisha siku ya Usafi Duniani. Picha TRT AFRICA

Maendeleo hayo mara nyingi huambatana na changamoto za uchafuzi wa mazingira, hivyo kufanya baadhi ya watu kubuni njia mbadala za kupunguza ongezeko la taka hasa zinazozalishwa mijini. Mabaki kama chupa na nyenginezo hukusanywa kwa ajili ya urejeleshaji viwandani.

Silvanius Pasco ni miongoni mwa waanzilishi wa kituo chaa kukusanya taka ngumu maarufu Dampo zikiwemo chupa za vinywaji mbalimbali kama soda, maji kabla ya kupelekwa viwandani kwa ajili ya urejeleshaji.

Wengi wametumia kama sehemu ya ajira, hupita mitaani na katika makazi ya watu kutafuta chupa ambazo baadae huuzwa na kujipatia kipato. Bei ya kilo moja huuzwa kwa shilingi 400 sawa 0.15 kwa dola. Silvanus mbali na kujisikia fahari kuwa sehemu ya wale wanaopunguza ongezeko la taka mjini lakini pia anaona ni sehemu ya ajira kwake.

Dunia inakabiliwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa taka hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira. Picha TRT AFRICA

“Najiskia vizuri kuwa miongoni mwa watu wanaosafisha mji na ninachokifanya kina faida na nani. Pia ukiacha usafishaji, kwetu nia ajira kwa sababu inatufanya tujikimu kimaisha,” alisema alipokuwa katika eneo la Soko la Machinga Complex jijini Dodoma ambapo mamlaka ya mji zilijumuika na wakaazi, wafanyabiashara na viongonzi mbalimbali wa kitaifa kwa lengo la kuitumia siku hiyo kuhamasisha jamii kuachana na utaratibu wa kienyeji wa kukusanya taka. Miongoni mwa wakazi walioshiriki ni pamoja na Othmani Ally ambae ni kiongozi wa wachuuzi katika soko la machinga Complex.

Othman alikiri kwamba elimu bado ni ndogo katika baadhi ya maeneo ikiwemo sokoni hapo ambapo ilionekana bado kuna changamoto ya baadhi ya watu kutupa taka maeneo yasio rasmi.

“Sisi sehemu kubwa inayozalisha taka za maji maji ni kwa mama lishe na wauzaji nyama, ingawa kuna sehemu ya kukusanya taka lakini watu hawazingatii utararibu wa kutupa taka na hiyo ni changamoto,” alisema Othaman.

Baadhi waliojitokeza wanaona fahari kushiriki katika zoezi hilo. Esta Mwaipopo ambae ni mfanyabiashara wa Soko hilo amejisikia fahari kuwa sehemu ya waliojumuika kufanya usafi akiwa na imani kwamba sehemu safi ndio chanzo ya kuvutia biashara.

“Nimefurahi kwa sababu kilele kimefanyika hapa na nimefurahi kuona kiongozi wa serikali akijumuika na sisi pia naamini kufanya usafi ni kivutio kwa biashara yangu na kwa wateja,” Ester aliiambia TRT Afrika.

Takwimu za uzalishaji taka jijini Dodoma zinaonyesha katika dampo la kisasa la Chidaya lenye ukubwa wa hekari 48 kwa siku hupokea tani 120 hadi 150 za taka ngumu kutoka katika vyanzo mbalimbali vya uzalishaji taka.

Hata hivyo uzalishaji huu wa taka ni mdogo ikilingalishwa na majiji makubwa kama vile Dar es Salaam ambapo kwa mwezi linazalisha tani zaidi ya laki moja za taka, huku jiji la Arusha kaskazini mwa Tanzania likizalisha tani takriban elfu tisa kwa mwezi huku kiwango kidogo tu kinachokwenda sehemu ya jalala.

Hata hivyo, uzalishaji huo unaacha maswali ya jinsi gani mamlaka zinazohusika serikalini zinajiandaa kukabiliana na hali hii kwa siku sijazo. Alipoulizwa swali hilo na TRT Afrika Dkt. Selemani Jafo ambae ni Waziri wa Mazingira nchini Tanzania alisema serikali lazima itenge kiasi cha fedha cha kununua mitambo ya kuzoa taka.

Ingawa juhudi hizi zinaleta matumaini, lakini maswali mengi bado yanasailia iwapo inatosha kwa hamasa kutolewa siku moja tu ya mwaka, au zoezi hili linatakuwa kuwa endelevu?

TRT Afrika