Takriban watu wanne walithibitishwa kufariki na waumini wengine 11 waliokuwa wamedhoofika kuokolewa kutoka kanisa lenye dhehebu ya kipekee katika Kaunti ya Kilifi nchini Kenya Ijumaa asubuhi.
Polisi walivamia kanisa hilo baada ya kupata kidokezo kutoka kwa wenyeji kwamba shughuli za kidini zinazoendelea katika kanisa ilo zilikuwa za ajabu na kwamba Kanisa la Good News International la Mchungaji Paul Mackenzie linasisitiza waumini kufunga na kutokula chakula hadi kupoteza uhai.
Taarifa ya polisi iliyotolewa kwa vyombo vya habari siku ya Ijumaa ilisema kuwa watu sita waliookolewa walikuwa wamedhoofika sana na wako katika hali mbaya.
Mchungaji mwenye kanisa amejificha. Alishtakiwa mwezi uliopita kwa kifo cha watoto wawili wachanga ambao walikufa kwa njaa na kwa sasa yuko huru kwa dhamana ya polisi.
Ripoti ya polisi ilifichua kuwa waathiriwa wanne, wanaume watatu na mwanamke, wote walikuwa waumini wa kanisa hilo. Polisi bado hawajatoa majina ya marehemu.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa madhehebu nchini Kenya. Baadhi ya madhehebu mapya nchini Kenya yamehusishwa na vitendo vya ukatili na uhalifu.