Machafuko yanayoendelea Mashariki mwa DRC yameua zaidi ya raia 7,000, Waziri Mkuu wa nchi hiyo alisema siku ya Jumatatu./Picha: Getty         

Machafuko yanayoendelea Mashariki mwa DRC yameua zaidi ya raia 7,000 katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari, Waziri Mkuu wa nchi hiyo alisema siku ya Jumatatu.

Kikundi cha M23 kinachodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kimeendelea kudhibiti maeneo yenye utajiri mwingi wa madini ikiwemo Goma na Bukavu.

"Hali ya kiusalama Mashariki mwa DRC ni ya kuugopesha,” amesema Judith Suminwa Tuluka, wakati akihutubia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Kulingana na Tuluka, vifo hivyo vinahusisha miili zaidi ya 2,500 ambao bado hawajatambulika na kuongeza kuwa miili mingine 1,500 ilikuwa kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti.

Alipoulizwa ikiwa waliokufa walikuwa ni wanajeshi tu, Tuluka alisema kuwa walishindwa kuitambua miili yote.

“Lakini ukweli ni kuwa watu wengi walipoteza maisha yao ".

Kulingana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa, kikundi cha M23 kinashikilia sehemu kubwa ya Mashariki mwa DRC.

TRT Afrika