DRC imekumbwa na ukosefu wa usalama wa miongo kadhaa, haswa katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo. / Picha: AFP

Waasi wenye mafungamano na itikadi kali wamewaua takriban wanakijiji 44 katika mashambulizi tofauti mashariki mwa Congo, viongozi wa serikali za mitaa na mashirika ya kiraia walisema Jumanne.

Waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) walishambulia kijiji cha Kishanga katika Mkoa wa Kivu Kaskazini Jumapili usiku na kuwaua watu 33, akiwemo askari wa jeshi la Congo, mjumbe wa gavana wa jimbo hilo, Samson Simara, alisema.

"Waasi waliwaua katika Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga," Simara alisema.

Waasi hao waliwaua wanakijiji wengine 11 katika jimbo la Ituri siku ya Jumanne, kulingana na Samuel Ngunjolo, kiongozi wa mashirika ya kiraia.

Mgogoro wa miongo kadhaa

"Tuna wasiwasi na tunaomba idara za usalama kupeleka usalama haraka," Ngunjolo alisema.

Sita kati ya waasi hao waliuawa na jeshi, kwa mujibu wa Kapteni Anthony Mulushayi, msemaji wa jeshi la Kongo huko Kivu Kaskazini. Baadhi ya mateka waliachiliwa, Mulushayi alisema.

Mashariki mwa Congo imekumbwa na mzozo kwa miongo kadhaa huku zaidi ya makundi 120 yenye silaha yakipigania udhibiti wa rasilimali muhimu za madini na baadhi kujaribu kulinda jamii zao.

Mauaji mengi yanayofanywa na waasi ni ya mara kwa mara. Ghasia hizo zimepelekea takriban watu milioni saba kuyakimbia makazi yao.

Mashambulizi yanaongezeka

Mashambulizi mabaya yameongezeka katika wiki za hivi karibuni huku mamlaka na vikosi vya usalama vikijitahidi kurejesha udhibiti na kupeleka wafanyakazi wa kutosha katika jamii ambako wengi wao ni wanawake na watoto wanalengwa.

Mapema mwezi huu, serikali ya Congo iliagiza kikosi cha kanda ya Afrika Mashariki, kilichotumwa mwaka jana kusaidia kumaliza mapigano, kuondoka nchini humo ifikapo mwezi Disemba baada ya kusema kwamba hakijaridhishwa na kazi yake.

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa pia umekabiliwa na shinikizo la kujiondoa kutoka DR Congo baada ya zaidi ya miongo miwili nchini humo.

TRT Afrika