Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo. Picha: Getty

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imeishinikiza Rwanda kusitisha msaada wote kwa waasi wa M23 na kujiondoa katika eneo la Congo.

Hata hivyo, Kigali imepuuza madai hayo na kusema haihusikia na M23.

"Kuhusu taarifa iliyotolewa leo na serikali ya Ufaransa juu ya hali ya Mashariki mwa DRC: Hakuna mtu anayejua zaidi kuliko Ufaransa sababu za msingi na historia ya mzozo Mashariki mwa DRC," msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo alisema, katika taarifa fupi iliyochapishwa kwenye Twitter (X) Jumanne.

Kwa miezi Kadhaa, DRC, Umoja wa Mataifa na baadhi ya nchi za Magharibi zimekuwa zikisema kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 katika jitihada za kudhibiti rasilimali kubwa za madini, madai ambayo Kigali siku zote imekuwa ikikanusha.

"Ikiwa masuala halisi katika asili ya mzozo unaoendelea yangeshughulikiwa, shida haingekuwepo," Yolande Makolo alisema.

Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yameonya kuwa mapigano hayo yanahatarisha kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika eneo la Mashariki mwa Congo.

Zaidi ya watu milioni 5 wamehamishwa katika majimbo manne ya eneo hilo kutokana na migogoro.

Aidha, Marekani imehimiza utulivu kwa pande zote mbili, huku Rais wa Angola Joao Lourenço akiteuliwa kuwa mpatanishi na Umoja wa Afrika (AU).

Wanamgambo hao wapo DRC Mashariki kwa miongo kadhaa, ngome ya vita vya kikanda vilivyopiganwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Baada ya miaka kadhaa ya kuwa kimya, M23 (Harakati ya Machi 23) ilichukua silaha tena mwishoni mwa 2021 na tangu wakati huo imechukua maeneo makubwa ya mkoa wa Kivu Kaskazini.

TRT Afrika na mashirika ya habari