Athari ya mafuriko katika mji wa Mai Mahiu / Picha: Reuters

Mafuriko na maporomoko ya ardhi kote nchini Kenya yamesababisha vifo vya watu 181 tangu Machi, huku maelfu wakilazimika kuacha makazi yao, serikali na shirika la msalaba mwekundu zilisema Jumatano.

Hali hiyo tete pia imeshuhudiwa Tanzania, Rwanda na Burundi. Wananchi wametakiwa wawe tahadhari na mvua kali inaondelea kunyesha.

Shirika la Rwanda linalosimamia rasilimali za maji limeonya kuwa mvua kubwa inayonyesha nchini humo huenda ikasababisha baadhi ya mito kupasuka kingo zake na kusababisha mafuriko.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Bodi ya Rasilimali za Maji ya Rwanda iliwashauri watu wanaoishi karibu na maeneo yanayokumbwa na mafuriko kuhama. Onyo hilo lilitolewa baada ya Shirika la Hali ya Hewa la Rwanda kuonya kuwa maeneo kadhaa ya Rwanda yatakabiliwa na mvua kubwa katika siku 10 za kwanza za Mei.

“Wakazi wanaoishi karibu na mito wanapaswa kuhama maeneo hatarishi na kuepuka kingo za mito wakati wa mvua kubwa,” ilisema taarifa hiyo.

Jumla ya watu 10 waliuawa kutokana na maafa yaliyosababishwa na mvua kubwa katika maeneo mbalimbali ya Rwanda katika siku 10 zilizopita za Aprili, Wizara inayohusika na Usimamizi wa Dharura ilitangaza Jumanne.

Halikadhalika Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania TMA imatangaza kuwepo kwa upepo mkali wa kilomita 40 kwa saa. Na hivyo kuwaomba wanachi kuwa makini.

TRT Afrika