Rwanda imetoa leseni kwa makampuni binafsi sita kwa ajili ya uzalishaji wa samaki aina ya Tilapia ambayo itauziwa wakulima wengine / Picha: Reuters

Uzalishaji wa samaki nchini Rwanda umeongezeka kidogo kutoka tani 46,495 mwaka 2023 hadi tani 48,133 mwaka 2024, hii ni kulingana na ripoti mpya ya Wizara ya Kilimo na Rasilimali za Wanyama (MINAGRI).

Rwanda ililenga kuzalisha tani 112,000 za samaki kila mwaka ifikapo 2024, kulingana na Mpango Mkakati wa nne wa Mabadiliko ya Kilimo (PSTA4), ambao utekelezaji wake ulianza mwaka 2018 hadi 2024.

"Ilihitajika tuzalishe tani 112,000 ili kufikia kiwango cha matumizi ya samaki kinachohitajika. Ingawa uzalishaji huu haukufikiwa kama ilivyotarajiwa, uliongezeka kwa kiasi kikubwa kulingana na njia na msaada uliopatikana," Solange Uwituze, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Kilimo na Rasilimali za Wanyama ya Rwanda alisema.

Uzalishaji ulikuwa tani 43,560 mwaka 2022 na tani 36,047 mwaka 2021.

Wizara ya Kilimo inasema Rwanda ilipata tani 32,756 mwaka 2020 na tani 31,465 mwaka 2019 na hivyo lengo la 2024 halijafikiwa kulingana na ripoti hiyo.

"Changamoto hizo ni pamoja na pembejeo za gharama kubwa za ufugaji wa samaki kama vile malisho na mbegu ambazo zilifanya kutokuwa na mvuto kwa wawekezaji ambao wangelazimika kuchukua jukumu muhimu kufikia lengo hilo. Changamoto nyingine zinazohusiana na sera na mfumo wa kisheria pamoja na usimamizi wa ufugaji wa samaki zilishughulikiwa hatua kwa hatua," Uwituze amesema.

"Lengo jipya la kitaifa ifikapo mwaka 2035 ni zaidi ya tani 106,000, ambapo takriban tani 80,620 zitatokana na ufugaji wa samaki na tani 26,000 kutoka kwa uvuvi wa kawaida," Uwituze alibainisha.

Katika hatua inayolenga kuimarisha ufugaji wa samaki nchini, Bodi ya Maendeleo ya Kilimo na Rasilimali ya Wanyama ya Rwanda (RAB) ilitoa leseni kwa viwanda sita binafsi vya kuzalisha samaki aina ya sato (tilapia) ili kusambaza tena kwa wafugaji wa ndani wa samaki.

Vitalu hivyo binafsi vilivyoidhinishwa vinapatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwa ni pamoja na Rwamagana, Kayonza, Bugesera, Gisagara na Rusizi, na vina uwezo wa kuzalisha mamilioni ya samaki wachanga kila mwaka.

TRT Afrika