Serikali ya Ethiopia imesema itaondoa usaidizi ambao inaweka katika mafuta na bidhaa husika.
"Serikali kwa sasa inatoa ruzuku ya 75% ya gharama ya mafuta ya dizeli na 67% ya gharama za 'benzene'. Hii inaweka bei ya mafuta nchini Ethiopia kuwa chini ikilinganishwa na nchi jirani kama Djibouti, Kenya, Uganda na Tanzania," amefafanua Waziri wa Biashara wa Ethiopia Abdulhakim Mulu.
Waziri alibainisha kuwa serikali inapanga kusitisha ruzuku hizi ndani ya mwaka mmoja, na kwenda kwenye mfumo wa upangaji bei unaoendeshwa na soko.
Kufuatia hayo kumekuwa na foleni ndefu katika vituo vya mafuta katika mji mkuu Addis Ababa, ambayo alamashauri ya jiji linasema haina maana.
Taasisi ya biashara ya Addis Abeba sasa imetoa onyo kuwa itavichukulia hatua vituo vya mafuta vilivyohusika kutengeneza foleni zisizo za lazima kufuatia tangazo lililopitishwa na bunge hivi karibuni kwa lengo la kudhibiti mfumo wa biashara ya bidhaa za petroli.
"Hakujawa na uhaba wa mafuta katika jiji katika kipindi cha miezi sita iliyopita," Habiba Siraj mkuu wa taasisi hiyo amesema .
Alisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya vituo vinavyojihusisha na mazoea kama vile kuuza mafuta kwa pesa taslimu pekee, kuleta upungufu kwa njia isiyo halali, au kushindwa kufanya kazi kwa muda wote.
Alisisitiza kwamba, kwa wastani, lita milioni 2 za dizeli na lita milioni 1.45 za petroli, ambayo ni jumla ya takriban lita milioni 3.45 za mafuta kwa siku, zimetolewa kwa vituo 125 vya mafuta katika jiji katika kipindi cha miezi sita iliyopita.