Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
"Mimi ni simulizi nzuri."
Hii ni mojawapo ya kauli mbiu za Doreen Moraa kwenye majukwaa yake ya mitandao ya kijamii.
Sio tu kujitia moyo bali pia kwa wengine wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) kuishi maisha ya kawaida.
Alizaliwa na virusi hivyo, hali yake iligunduliwa tu akiwa na umri wa miaka 13.
"Miaka 31 ya kuwa mwathirika wa VVU, miaka 18 ya kutumia ARVs, miaka 23 tangu kugunduliwa kwangu rasmi na VVU na bado niko hapa. Mimi bado ni simulizi nzuri. Na kuvipa nafasi virusi vidogo visivyoweza kuongea," anaandika kwenye mtandao wake wa kijamii wakati Dunia inaadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani.
Kila siku Moraa ana shughuli za kufanya ili kuleta mabadiliko katika jamii nchini Kenya na kwengineko. Yeye ni mtetezi wa kuzuia na kuhamasisha matibabu ya VVU.
Karibu kila siku yeye huchapisha picha na maoni yake ambayo yanasisitiza jinsi alivyo wa kawaida.
"Kitaalamu, hakuna kinachobadilika kuhusu maisha yako kama mtu unayeishi na VVU kutokana na ukweli kwamba unapaswa kupata matibabu kila siku huku maisha yakiendelea kama mtu ambaye hana VVU," anaiambia TRT Afrika.
"Hata hivyo, sisi katika Afrika bado hatujafanya mazungumzo kuhusu VVU kuwa ya kawaida mpaka kufikia mwaka wa 2023," Moraa anasema ujumbe wake katika mitandao unasaidia wale ambao bado wanateseka na unyanyapaa katika jamii.
Yeye ni kati ya zaidi ya watu milioni 1.12 walio katika mpango wa dawa za kurefusha maisha nchini Kenya yaani ARV.
Kulingana na Baraza la Kitaifa wa Kudhibiti Magonjwa ikiwemo Ukimwi, kuna zaidi ya watu milioni 1.4 wanaoishi na VVU nchini.
Uhaba wa madawa
Moraa alikuwa kati ya waliopaza sauti mwaka wa 2021 wakati Kenya ikikabiliwa na upungufu wa dawa za ARV baada ya shehena ya mizigo kukwama katika bandari ya Mombasa.
Hali iliyochangiwa na msuguano ulioibuka kati ya serikali ya Kenya na ile ya Marekani ambayo ndio mfadhili mkuu wa dawa hizo.
Kenya ilikuwa imeitaka kampuni binafsi ya Marekani, Chemonics, ambayo ilikuwa imeleta dawa hizo kutoka nje kwa niaba ya USAID ilipe ushuru wa thamani ya $587,275.
"Kwa bahati mbaya, tunategemea sana wafadhili katika bidhaa zote zinazohusiana na matunzo na matibabu ya VVU na hilo ni tatizo kwa sababu inaleta changamoto ya utegemezi," anaiambia TRT Afrika.
"Na sasa tumeona changamoto ya maandalizi baada ya janga la UVIKO 19, kipaumbele cha wafadhili kwa VVU kinaonekana kubadilika. Kwa hiyo hapo ndipo joto lilipo,” anasema.
Tukivuka mpaka huko Uganda, Rose Sanyu na anaonyesha wasiwasi wake katika upatikananaji wa dawa.
Miaka 45 ya kutumia ARV
Mwezi Mei, 2023, Marekani ilitangaza azma ya kusitisha mpango wa ufadhili wa ARVs Uganda chini ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) baada ya Uganda kuamua kupitisha sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja.
"Tulifanya makubaliano tulipoanza kutumia dawa za ARV kwamba hatukusita kamwe," Sanyu anaelezea TRT Afrika, "Siwezi kuruka hata siku moja kwa sababu virusi vyangu vitaongezeka. Ni lazima ninywe dawa kila siku saa tatu usiku bila kukosa.”
Kati ya zaidi ya watu milioni 1.4 walioathiriwa na VVU nchini Uganda, zaidi ya milioni 1.3 wanategemea msaada wa ARV kutoka PEPFAR.
"Kwa bahati mbaya, dawa zetu zote, tunaambiwa, zinatoka nje ya nchi. Tunahitaji kuhakikishiwa kwamba serikali itashughulikia usambazaji bila kushindwa," amesema.
Ingawa Marekani haikutekeleza mpango wake wa kusitisha ufadhili huo, lakini serikali imeamua kuangalia zaidi ufadhili wake wa dawa hizo.
Tume ya Taifa ya Ukimwi nchini Uganda, inasema inagharimu takriban dola 184 kutoa matibabu ya ARV kwa mtu mmoja kwa mwaka.
Hivi sasa, pendekezo lililopo kutoka bungeni ni utekelezaji wa Mfuko wa Udhamini wa VVU/UKIMWI ulioanzishwa mwaka wa 2014, huku fedha hizo zikilengwa katika ushuru wa vinywaji.
Tume ya UKIMWI ya Uganda imewahakikishia raia kwamba kamwe hawatakosa dawa.
Matumaini ya Kuzuia maambukizi zaidi
Huku ikilenga kukomesha virusi vya Ukimwi ifikapo mwaka 2030, Uganda ina wasiwasi wa kuongezeka kwa maambukizi mapya.
Mwaka 2022, kulikuwa na maambukizi mapya 52,000 hasa miongoni mwa vijana.
Nchi hiyo imetangaza kuanza matumizi ya Cabotegravir (CAB-LA), dawa ya kurefusha maisha kupitia sindano kuanzia mwaka wa 2024.
Iliidhinishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni mnamo Julai 2022 kama "chaguo la ziada la kuzuia VVU kwa watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU."
"Tunalenga watu 10,000 katika mwaka wa kwanza, na tunaongeza kwa 10,000 katika miaka inayofuata ili kufaidika na hili. Lakini kama mahitaji ni makubwa sana, ninaahidi kwamba tutaiwezesha kupatikana,” alielezea Dkt. Daniel Byamukama, mkuu wa Kinga ya VVU katika Tume ya Ukimwi Uganda.
Kulingana na WHO, mtu anafaa kupata sindano mara moja kila mwezi kwa miezi miwili ya kwanza. Baada ya hapo, atapokea sindano ya cabotegravir mara moja kila baada ya miezi 2.
Malawi, Zambia na Zimbabwe ni baadhi ya nchi zilizothibitishwa kupokea dawa hizo.
Kwa upatikanaji zaidi wa dawa hizo, kampuni ya dawa yenye makao yake makuu nchini Uingereza ya ViiV Healthcare, imeidhinisha utengenezaji wa dawa za muda mrefu za PrEP kwa nchi 90.
Lakini hili litachukua muda kutekelezwa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Ukimwi UNAIDS, limeitaka kampuni ya ViiV kupunguza gharama ya sindano za CAB-LA katika nchi za kipato cha chini.
Imependekeza “bei iwekwe karibu na gharama ya sasa ya tembe za PrEP—ambayo ni takriban $60.”
Lakini hata ikipunguzwa kwa bei wanaharakati dhidi ya maambukizi ya VVU kama Moraa, anataka serikali za Kiafrika kuweka mikakati ya kutumia zaidi rasili mali zao wenyewe kwa ununuzi wa dawa.
"Ni muhimu serikali zetu sasa kujitolea kikamilifu. Je, ni nani atasimamia gharama ya kupata sindano hii kwa watu?"
Na huku wito ukitolewa kwa serikali za Afrika, wataalamu wanashauri ni muhimu watu kuwajibika binafsi kwa kujua hali yako, kujikinga, na iwapo umepata maambukizi, basi tumia dawa.