Wasomi na wadau kutoka seriklai na sekta binafsi kutoka nchi za Afrika Mashariki na kati wanakutana jijini Yaounde, Cameroon, kujadili jinsi uvumbuzi na utafiti unavyoweza kuchochea Ushirikiano wa kikanda.
Kamati ya Kiserikali ya Maafisa wakuu na Wataalamu (ICSOE) imeandaliwa na Tume ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika, UN ECA.
Jukwaa hilo linatoa fursa ya kubadilishana mawazo ya namna ushirikiano wa kikanda unaweza kuchukua hatua kuu kutoka kwa wataalamu kutoka nchi 20 barani Afrika.
"Ubunifu ni muhimu kwa tija. Ni lazima tuongeze juhudi zetu, tutengeneze mazingira wezeshi ya kibiashara na kujenga ujuzi wa teknolojia kwa wananchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini na ukosefu wa usawa," Hanna Morsi, Katibu mkuu wa UN ECA alisema.
Athari za Uviko 19
Ripoti iliyotolewa mwezi huu na Kamisheni ya Uchumi ya Afrika inaonesha kuwa tangu 2020, ukuaji wa uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki umeathirika na athari za janga la Uviko-19 na mzigo mkubwa wa madeni.
Uchambuzi unaonesha kupungua kwa matumizi ya serikali katika nchi nyingi.
"Uwekezaji wa sasa wa Afrika katika utafiti na maendeleo ni asilimia 0.42 tu ya Pato la Taifa iko nyuma ya viwango vya kimataifa ambavyo lazima virekebishwe. Wastani wa kimataifa ni asilimia 1.7," alisema Claver Gatete, Katibu Mtendaji wa Tume ya Uchumi UN.
Majadiliano hayo yanaendelea wakati bara la Afrika linaendelea kujitahidi kutimiza biashara ndani ya mpango wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
Kukuza utalii
Wataalamu wanasema bara hilo linahitaji kujiinua kupitia uwezo wake hasa kupitia sekta za utalii.
"Utalii ndio unaochochea biashara," anaeleza Geoffrey Manyara, mtaalam wa utalii kutoka ECA.
"Nikupe mfano tu, mmoja wa wasafirishaji wakuu nchini Rwanda alikuja kwanza kama mtalii lakini akagundua kuwa kulikuwa na fursa huko. Sasa yeye ni mmoja wa wasafirishaji wakuu. Kwa hivyo tunahitaji kukuza utalii kote Afrika," anaongeza.
Mataifa ya visiwa
Mojawapo ya nguvu zinazosukuma Ushirikiano wa Kikanda ni Mkataba Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika ambao nchi nyingi za visiwani zitaridhia.
"Nadhani tunahitaji kuwa na chapa yetu kutoka Ushelisheli," anaelezea Pierre Michel Mtaalam wa Sekta ya binafsi kutoka visiwa vya Shelisheli.
"Jambo moja ambalo ningependa kutaja ni usalama. Kwa mfano unapozungumzia Afrika, baadhi ya watu wanasema si salama, tunatakiwa kuachana na dhana hii, twende pamoja tuache Afrika iwe salama,” anaongeza.
Wataalamu wengine wamependekeza haja ya kujumuisha zaidi vijana katika nyanja zote za utafiti na maendeleo.
Fursa za uvumbuzi
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu asilimia 70 ya wakazi wa Afrika wana umri chini ya miaka 30.
Vijana, wanaojulikana kwa ubunifu na ujuzi wao, hasa katika mitandao, ni muhimu katika Utangamano wa kikanda, lakini jinsi wanavyoweza kutumia fursa za ugunduzi wao, unabakia kuwa changamoto kubwa.
"Kimsingi mimi huwa nafikiri vijana wanahitaji kupewa matumaini. Hili litawazekana iwapo watawezeshwa kisiasa, kijamii na kiuchumi," Johnson Rithaa kutoka Baraza la Kitaifa la Vijana la Kenya anasema.