Wasira anachukua nafasi ya Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana ambaye alijiuzulu wadhifa huo mwaka jana./ Picha: ukurasa wa X , Mwanga TV

Mkutano mkuu wa kitaifa wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi CCM, kimemteua Stephen Wasira kama Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara katika shughuli iliyofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma.

Kufuatia uteuzi huu, Wasira anachukua nafasi ya Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana ambaye alijiuzulu wadhifa huo mwaka jana.

Wasira ni miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa zaidi ndani ya CCM, ambapo amewahi pia kushikili anafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na pia alihudumu kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

Katika kupokea uteuzi wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa ana imani Wassira anaweza kuitetea CCM na taifa la Tanzania.

''Katika kujaza nafasi hii, kamati kuu na halmashauri kuu ya taifa tulikaa tukaangalia wana CCM ambao wanaweza kujaza nafasi hii, na tukampata mmoja ambaye ni mbobezi lakini yuko tayati kuvua shati, kufungua kifua kukingia CCM, naye ni mzee wetu Stephen Wassira,'' alisema Rais Samia.

Stephen Wassira anaungana na mwenzake Dkt Hassan Mwinyi, ambaye ndiye Makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar wote wakihudumu kama washauri na wasaidizi wa Mwenyekiti wa CCM kitaifa ambaye pia ndiye Rais wa Taifa , Samia Suluhu Hassan.

TRT Afrika