Ghasia zimelikumba taifa hilo la kusini mwa Afrika tangu chama cha Frelimo, ambacho kimetawala kwa takriban miaka 50, kushinda uchaguzi wa Oktoba 9 / Picha: Reuters

Wanajeshi na polisi walishika doria katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, mapema Alhamisi kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanyika kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyokataliwa na upinzani.

Ghasia zimelikumba taifa hilo la kusini mwa Afrika tangu chama cha Frelimo, ambacho kimetawala kwa takriban miaka 50, kiliposhinda uchaguzi wa Oktoba 9.

Jiji la zaidi ya watu milioni moja lilikuwa katika hali tete siku ya Alhamisi asubuhi, ambapo maduka, benki, shule na vyuo vikuu vilifungwa. Maelfu ya waandamanaji walikusanyika kwenye moja ya barabara kuu kabla ya kuamrishwa na askari kurudi nyumbani.

Matokeo yanayobishaniwa

Daniel Chapo wa Frelimo alishinda uchaguzi wa urais kwa asilimia 71 ya kura, kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, huku mgombea mkuu wa upinzani Venancio Mondlane akiibuka wa pili kwa asilimia 20.

Mondlane, akiungwa mkono na chama cha Podemos na ambaye alisema matokeo yalikuwa ya uongo na kwamba yeye ndiye aliyeshinda, aliitisha maandamano makubwa siku ya Alhamisi.

Kwa kutumia mitandao ya kijamii, amewakusanya wafuasi wake barabarani tangu uchaguzi katika maandamano ambayo yamezua vurugu kutokana na ukandamizaji wa polisi.

Katika mahojiano na shirika la Habari la AFP, kiongozi huyo wa upinzani ambaye hajulikani aliko, alisema hatakuwepo kwenye maandamano hayo kutokana na wasiwasi wa usalama wake.

Takriban 18 waliuawa

Takriban waandamanaji 18 wameuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi, kulingana na Human Rights Watch.

Kituo cha Demokrasia na Haki za Kibinadamu (CDD), kilisema idadi ya vifo ilikuwa 24.

Afisa wa polisi pia aliuawa katika maandamano mwishoni mwa juma, Waziri wa Ulinzi Cristovao Chume akiwaambia waandishi wa habari Jumanne kuwa, jeshi linaweza kuingilia "kulinda masilahi ya serikali."

"Kuna nia ya kubadilisha mamlaka iliyoanzishwa kidemokrasia," alisema, huku kukiwa na hofu kwamba Rais anayemaliza muda wake Filipe Nyusi anaweza kutangaza hali ya hatari.

Nyusi anatarajiwa kuachia ngazi mapema mwaka ujao mwishoni mwa muda wake wa mihula miwili.

Vizuizi vya mtandao

Mamlaka imezuia ufikiaji wa mtandao kote nchini katika kile kinachoonekana kama juhudi za "kukandamiza maandamano ya amani na ukosoaji wa serikali," kulingana na Human Rights Watch (HRW).

"Kuzimwa kunazuia uwezo wa watu kupokea na kutumia taarifa zinazookoa maisha, kukusanyika kwa amani, na kutoa maoni yao ya kisiasa katika wakati wa mgogoro," Allan Ngari, alisema Mkurugenzi wa utetezi wa Afrika kutoka HRW.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, alisema Jumatano kwamba "ametiwa hofu sana na ripoti za ghasia kote nchini."

"Polisi lazima wajizuie kutumia nguvu zisizo za lazima au zisizo na uwiano na kuhakikisha kwamba wanasimamia maandamano kulingana na wajibu wa kimataifa wa haki za binadamu wa Msumbiji," alisema.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika imetoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa kilele usio wa kawaida kati ya Novemba 16 na 20 kujadili maendeleo nchini Msumbiji.

TRT Afrika