Kurejea kwa wanajeshi hao wa KDF kuliashiria kilele cha miezi 12 ya huduma ya kujitolea na vilivyowekwa chini ya kikosi cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) ili kudumisha amani na utulivu katika Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kikosi cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichojumuisha wanajeshi kutoka Kenya, Burundi, Uganda, na Sudan Kusini, kilianza kujiondoa DR Kongo, mapema Disemba.
Wanajeshi kutoka mataifa hayo walianza kuondoka baada ya serikali ya Kongo kufanya uamuzi wa kutorefusha tena mamlaka yake, uamuzi ambao uliwasilishwa kwenye mkutano wa kilele wa EAC mnamo Novemba 24.
Kikosi cha EACRF kilitumwa kudumisha utulivu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo Novemba 2022 kwa kukabiliana na waasi wa M23 walioteka maeneo mengi na kuzua changamoto za kiusalama.
Mashariki wa DR Kongo inajulikana kuwa na zaidi ya makundi 130 yenye silaha za ndani na nje ya nchi.
Akizungumza baada ya kuwapokea wanajeshi hao, mkuu wa majeshi ya Ulinzi Jenerali Francis Ogolla, ameahidi kuwa wanajeshi wa KDF wataendelea kuunga mkono juhudi za vikosi vya amani wakati wowote itakapoitwa.
Ogolla alibainisha kuwa juhudi za wanajeshi wa Kenya na vikosi vya kikanda zimeonyesha uwezo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kushughulikia changamoto za usalama kwa pamoja katika eneo nzima.