Polisi nchini Senegal wakipambana na waandamanaji wanaopinga kuchelewesha kwa uchaguzi. Picha: Reuters

Hatua ya Rais Macky Sall ya kuahirisha uchaguz wa Februari 25 hadi Disemba uliitumbukiza Senegal katika mgogoro ambao umesababisha vifo vya watu watatu kwenye makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

"Kutokana na usambazaji kwenye mitandao ya kijamii wa ujumbe kadhaa wa chuki ambao tayari umesababisha maandamano ya vurugu... mawasiliano ya rununu yamesimamishwa Jumanne 13, Februari," Wizara ya Mawasiliano ya Simu imesema katika taarifa yake.

Upatikanaji wa taarifa ya simu tayari ulikuwa umepunguzwa kwa muda wa siku nane zilizopita wakati bunge lilipounga mkono uamuzi wa Sall wa kuahirisha uchaguzi.

Uamuzi huo ulikosolewa vikali na wanaharakati wa haki za Binadamu na washirika wakuu wa Kimataifa wa Senegal, wakiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya.

Hatua ya kukata mawasiliano ya mtandao wa simu ilikuwa ni marudio ya hatua ya Juni mwaka uliopita, ambapo serikali ya Senegal ilizuia usambazaji huku kukiwa na mvutano mkubwa nchini humo.

Hatua hiyo imekuwa ya kawaida ya kuzuia uhamasishaji na mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii, ikilaumiwa vikali na wanaharakati.

AFP