Mwaka huu kuna jumla ya watahiniwa 965,501, ongezeko kutoka 903,138 mwaka 2023./ Picha : @AfricaFirsts

Wanafunzi wa kidato cha nne nchini Kenya wameanza mitihani yao wa mwisho (KCSE) baada ya miaka minne ya masomo.

"Kila la heri kwa watahiniwa 965,000 watakaofanya mtihani wa KCSE unaoanza leo. Juhudi na maandalizi yao ya miaka minne yaweze kuzawadiwa kwa mafanikio," Rais William Ruto wa Kenya amesema katika akaunti yake ya X.

Mitihani ya mwaka huu itafanywa na watahiniwa 965,501, ongezeko kutoka 903,138 mwaka 2023.

Kifaransa, Kijerumani, Lugha ya Ishara, Kiarabu, Muziki na Sayansi ya Nyumbani zitatawala wiki ya kwanza ya mitihani, itakayofanywa katika vituo 10,755 kote nchini.

Wizara ya Elimu Oktoba 4 ilitoa miongozo mipya itakayoongoza tathmini ya mwaka huu.

Hii ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mzunguko wa wasimamizi wa vituo ambao hawataruhusiwa kuwepo katika kituo cha mitihani kwa zaidi ya wiki moja.

Simu za wasimamizi za mkononi zitasalia mahali penye ulinzi mbali na vyumba vya mitihani.

Watahiniwa watakuwa na karatasi za maswali za kibinafsi.

Mtihani wa KCSE utaendeshwa sambamba na Tathmini ya Elimu ya Shule za Msingi nchini Kenya (KPSEA), itakayoanza Oktoba 28, huku zaidi ya watahiniwa milioni moja wakitarajiwa kufanya tathmini hiyo.

TRT Afrika