Kenya imepokea kundi la kwanza la wananchi wake walio okolewa kutoka Sudan. Takriban siku kumi tangu kuzuka mapigano katika mji mkuu Khartoum. Wanafunzi 39 waliwasili mjini Nairobi baada ya kuopolewa kwa ndege ya kijeshi ya Kenya kutoka nchi jirani ya Sudan Kusini.
Akihutubia wanahabari baada ya kuwapokea wanafunzi hao katika uwanja wa ndege wa JKIA jijini Nairobi, Waziri wa Ulinzi, Kenya, Aden Duale alisisitiza kuwa watatoa kipaumbele katika kuwaokoa wananchi wao.
“Serikali imejitolea kuhakikisha kurudishwa salama kwa Wakenya wote wanaotaka kurudi nyumbani kutoka Sudan.” Duale alisema.
Kuna zaidi ya wakenya 3000 nchini Sudan wakiwemo wanafunzi, wafanyakazi au watalii. Chini ya wiki moja tangu kuanza kwa vita nchini Sudan, Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya ilitangaza kuundwa kwa kikosi maalum kitakachowajibikia kutoa msaada kwa wananchi wake huko, ikiwemo kuondolewa kwa dharura.
Hata hivyo baadhi ya wanafunzi waliokwama nchini Sudan wameelezea katika mitandao ya kijamii wasiwasi wao juu ya namna zoezi la uokoaji unavyofanyika.
Mmoja wao @Aylaizayla aliandika katika Twitter “ Tusipouawa kwa risasi basi tutakufa kwa kiu na njaa. Mungu tuepushe....... Tumekuwa tukisubiri muda mrefu na tumechoka.”
Mwingine @Asinat Noor amesema “ Wengine wetu bado tupo mjini Khartoum. Tunaishiwa na mahitaji muhimu, tunahofia maisha yetu tafadhali tushughulikieni kwa dharura.”
Wakati huo huo Waziri wa Ulinzi, Kenya, Aden Duale amewataka wakenya wanaohitaji msaada nchini Sudan, kuwasiliana kupitia nambari za dharura zilizotolewa.
Vyuo vikuu nchini Sudan vina idadi kubwa ya wanafunzi kutoka nchi jirani hasa barani Afrika, zikiwemo Kenya, Tanzania, Ethiopia na Somalia.