Viongozi wa nchi wanachama wa Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo, IGAD katika mkutano wao nchini Djibouti wamechambua usalama katika eneo lao.
Nchi wanachama wa IGAD ni Kenya , Somalia, Uganda, Djibouti, Sudan Kusini , Ethiopia na Eritrea.
Viongozi wamekashifu kuendelea kwa vita nchini Sudan tangu tarehe 15 Aprili wakati mzozo ulianza kati ya Jeshi la Sudan na wanajeshi chini ya kikundi cha Rapid Support Forces, RSF.
"IGAD inatoa wito kwa pande zote kusitisha uhasama na kutoa fursa ya mazungumzo. Ni fursa ya kuzuia upotezaji zaidi wa maisha na kuruhusu uhamishaji salama wa raia wanaotaka kutoroka mapigano," Workneh Gebeyehu, katibu mtendaji wa IGAD amesema.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika , Moussa Faki Mahammat , kwa upande wake ameongea vikali akisema kuna maneno mengi potovu yayayoongelewa kuhusu Umoja wa Afrika na Sudan .
Hajasema maneno hayo yamesemwa na nani.
Faki anasema Umoja wa Afrika utaipa msaada Sudan , ila tu kwa wito wa Sudan yenyewe.
"Tunaunga mkono mazungumzo ya kipekee yaliyoundwa na kuongozwa na Wasudan wenyewe mbali na kuingiliwa kati na watu wowote wa nje, " Faki alielezea mkutano wa IGAD.
Je mpango wa Umoja wa Afrika ni nini kwa Sudan ?
Mamlaka ya IGAD iliteuwa Kenya, Djibouti na Sudan Kusini kuongoza juhudi za mapatanisho kati ya majenerali wa Sudan, Abdel Fattah al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo ambao wamekuwa na mzozo tangu Aprili.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya majenerali wa Marekani yaliyosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia hayajakuwa na mafanikio mara kwa mara.
Katika mkutano wa baraza la amani na Uslama la Umoja wa Afrika , uliofanyika tarehe 27 Mei mwaka huu, Umoja wa Afrika uliamua kuweka mkakati wa kuisaidia Sudan .
Mkutano huu uliongozwa na rais Yoweri Museveni wa Uganda, ukitoa imani kwa Sudan kuwa na uwezo wa kuongoza suluhisho yao wenyewe,
"Kwa nini baadhi ya watu wanasema kwamba Sudan haijajumuishwa katika utaratibu huu? Jibu ni rahisi sana na mara nyingi wanaouliza wanajua jibu kama sisi," Faki, mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika aliambia mkutano wa IGAD.
"Sudan imesimamishwa kutohusika katika maswala ya Umoja wa Afrika na chombo pekee chenye mamlaka barani katika suala la amani na usalama barani , na hiyo ni baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika, " alisema.
Katiba ya Umoja wa Afrika inasema kuwa nchi ambazo zimehusika katika mapinduzi ya kijeshi haziruhusiwi na haziwezi kuhusika katika mikutano yoyote ya Umoja wa Afrika hadi hapo hali ya uongozi wa kawaida itakaporejea kupitia uchaguzi.
"Mgogoro nchini Sudan upo katika kiwango ambacho hairuhusu mgawanyiko wowote kati yetu ," Faki ameongezea, " ni muhimu kupunguza uingiliaji wa kigeni."