Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyoko jijini Arusha nchini Tanzania./Picha: EAC

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) watakutana mtandaoni Juni 7, 2024 katika Mkutano wa 23 wa Jumuiya hiyo yenye nchi wanachama nane.

Kikao hicho, ambacho kitakuwa chini ya uenyekiti wa Salva Kiir Mayardit, Rais wa Sudan Kusini, pia kitapitisha jina la Jaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), ambaye pia anatoka Kenya.

Serikali ya Kenya imependekeza jina la Veronica Mueni Nduva kuchukua nafasi ya Caroline Mwende Mueke katika nafasi ya Katibu Mkuu wa EAC.

Ikumbukwe kuwa, jina la Mueke lilipendekezwa na Rais wa Kenya, William Ruto kama mbadala wa Peter Mutuku Mathuki, ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Urusi.

Mueke alitarajiwa kumaliza kipinchi cha miaka miwili cha uongozi wa mtangulizi wake.

Hata hivyo, Aprili 15, 2024, Serikali ya Kenya ilipitisha jina la Veronica Mueni Mwende kama mbadala wa Mweke ndani ya EAC.

Kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria, Katibu Mkuu wa EAC, anapaswa kuhudumu kwa kipindi cha miaka 5. Hata hivyo, Mathuki alikuwa amehudumu kwa miaka 3, katika nafasi hiyo ya juu ndani ya EAC, kabla ya maamuzi ya Machi 8, yaliyofikiwa na Rais Ruto.

Kulingana na itifaki ya kuanzisha EAC, Rais wa nchi husika anaweza kupendekeza jina kwa nafasi ya Katibu Mkuu, kabla ya kuidhinishwa na Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki.

TRT Afrika