Profesa Kithure Kindiki./Picha: Reuters  

Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Kenya imetangaza Novemba 1, 2024 kama siku ya mapumziko ili kuruhusu zoezi la kumuapisha Kithure Kindiki kama Naibu Rais wa nchi hiyo.

Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Musalia Mudavadi, amesema uamuzi huo unatoa nafasi kwa wakenya kushuhudia tukio la kuapishwa kwa Naibu Rais mteule Kithuri Kindiki.

Zoezi la kumuapisha Profesa Kindiki linatarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa Kenyatta (KICC) jijini Nairobi.

Mnamo Oktoba 17 mwaka 2024, bunge la Seneti la nchini Kenya lilipitisha kura ya kumuondoa madarakani aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua.

Hatua hiyo, ilimlazimu Rais William Ruto kumteua Waziri wa Mambo ya ndani wa nchi hiyo, Kithure Kindiki kuchukua nafasi ya Gachagua, kabla ya Mahakama kupinga uteuzi huo.

TRT Afrika