Serikali ya Kenya imeahidi kuimarisha hatua za kiusalama dhidi ya wanamgambo wa Al Shabaab wakati ikiadhimisha miaka kumi tangu shambulio mbaya la maduka ya Westgate jijini Nairobi.
"Lengo letu ni kudumisha kiwango cha juu zaidi cha usalama katika mipaka yetu na operesheni za usalama kote nchini, na kuwazuia maadui kabla hajashambulia," Raymond Omollo, afisa mkuu wa wizara ya mambo ya ndani alisema Alhamisi katika taarifa yake ya maadhimisho ya miaka 10 ya mashambulizi hayo.
Maafisa wa serikali waliweka maua meupe na mekundu ya waridi nje ya lango kuu la maduka ya Westgate kwa heshima ya waathirika wa shambulio hilo.
Ni nini kilijiri Westgate 2013?
Mnamo Septemba 21, 2013, watu wanne waliokuwa wamejifunika nyuso zao kwa bunduki walishambulia jumba la maduka maarufu Westgate jijini Nairobi.
Watu hao walisimama kwenye lango kuu la Westgate Mall, wakiendesha gari aina ya Mitsubishi Lancer yenye namba za usajili KAS 575X.
Inaripotiwa walianza kurusha mabomu na kuwafyatulia watu risasi.
Baadhi waliweza kukimbia na wengine kuwasaidia wananchi wengine kutoroka kutoka kwenye eneo la tukio.
Washambuliaji walidai kuwa shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi kwa Kenya kutuma wanajeshi wake nchini Somalia mwaka 2011 na kupambana na wanamgambo wa al Shabaab.
Kwa mujibu wa serikali ya Kenya, shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 67 huku ikidai kuwaua washambuliaji wote waliohusika.