Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Mara nyingi tunawaona wakisimama nyuma ya Marais na wakuu wengine wa nchi, wakiambatana nao popote pale waendapo.
Je, umeshawahi kujiuliza hawa ni akina nani?
Jibu ni rahisi; hawa ni wapambe wa Marais, au kwa lugha ya kimombo hujulikana kama ‘aide-de-camp’, likiwa na maana ya 'Msaidizi'.
Wakiwa wamevalia sare za kijeshi, wapambe hawa hudhaniwa kuwa ni walinzi wa Marais.
La hasha. Kazi kubwa ya watu hawa ni kuwasaidia Marais, hasa wanapokuwa kwenye shughuli za kitaifa na za kimataifa.
Tofauti na walinzi wa Rais, ambao wanajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa Rais anakuwa salama dhidi ya hatari zozote zitakazoweza kumkabili awapo hadharani au hata kwenye makazi yake binafsi, wapambe wa Marais huwa na wajibu wa kumsaidia kiongozi huyo awapo kwenye shughuli mbalimbali.
Wakati walinzi wa Rais huwa wamebeba silaha, wapambe wa Marais hutembea bila silaha, licha ya kuwa na mavazi ya kijeshi.
"Wapambe wa Marais huchaguliwa kutoka kwenye majeshi ya ulinzi wa nchi husika kupitia vigezo mahsusi," Daniel Theuri, mchambuzi wa mambo ya ulinzi na usalama kutoka Kenya anaiambia TRT Afrika.
Kwa mujibu wa Theuri, mara nyingi ya wapambe wa Marais huwa na vyeo vya Makanali yaani nyota mbili katika nchi za Jumuiya ya Madola, na huicha kazi hiyo mara baada ya kuongezeka cheo.
Kwa mfano, aliyewahi kuwa Mpambe wa Rais wa wakati utawala wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na John Pombe Magufuli wote wa Tanzania, Mbaraka Mkeremi, alichana na majukumu hayo, mara baada ya kupanda cheo na kuwa Meja Jenerali.
Mwezi Julai mwaka 2024, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alimpandisha cheo Mpambe wake wa sasa Kanali Nyamburi Mashauri hadi kuwa Brigedia Jenerali.
Hii inamaanisha kuwa, kiongozi huyo atapata mtu mwingine wa kusimama nyuma yake mwenye cheo cha Kanali, huku Brigedia Jenerali Mashauri akiendelea na majukumu mengine.
Wakati tumezoea kuwaona Marais wengi wa kiume wakiwa na wapambe wao wa kiume, pia ni jambo la kawaida kabisa kwa Rais wa kiume kuwa na mpambe wa kike na Rais wa kike, pengine kuwa na mpambe wa kiume.
Mfano mzuri ni nchini Kenya, ambapo Mpambe wa Rais William Ruto ni Luteni Kanali Damaris Agnetta.
"Uchaguzi wao watu hawa hufanyika kwa uangalifu mkubwa sana kwani mpambe wa Rais anakuwa kiungo muhimu kati ya Rais ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa nchi na Jeshi la nchi hiyo," anaeleza.
Kwa mfano, kama itatokea Mkuu wa Majeshi wa nchi fulani atahitaji kupitisha ujumbe wa dharura kwa Rais, basi ni lazima apitie kwa Mpambe huyu.
Hii, ina maana kwamba, lazima mteuliwa awe na uelewa mkubwa wa mambo yanayohusu majeshi, kama vile vyeo, majukumu na mengineyo.
Wakati Wapambe wa Marais huchaguliwa kutoka majeshi ya Ulinzi, walinzi wa Rais, ambao mara nyingi humzunguka kiongozi huyo, hutoka kwenye majeshi ya Polisi, wakiwa wamepitia mafunzo maalumu ya ulinzi.
"Mpambe wa Rais huwa anapewa ofisi yake maalumu ndani ya jengo la Ikulu, ili kumuwezesha kuratibu shughuli nzima za siku nzima za Rais, kumbebea nyaraka kazi na vitu vingine vya binafsi," anasema Theuri.
Mpambe wa Rais anajukumu la kufahamu ratiba nzima ya siku ya Rais, akijua atakutana na nani, wapi na kwa muda gani.
Kifupi, Mpambe wa Rais anajukumu la kusimamia itifaki ya siku nzima ya Rais husika.
"Yeye ndio mwenye kubeba begi la Rais, na mara nyingi begi hilo huwa na nyaraka muhimu, kama vile hotuba, nakala ya katiba, fedha na pengine vifaa vya mawasiliano vya Rais," anaongeza.
Kama ulikuwa hujui, Mpambe wa Rais pia anahusika kwa namna moja au nyingine kujua ni mavazi gani na kwa wakati gani atayavaa.
Wakati fulani, Rais wa zamani Mwai Kibaki aliwahi kupatwa na kadhaa yenye kufedhehesha wakati anatoa hutoba yake.
Hata hivyo, aliyekuwa Mpambe wake kwa wakati huo Kanali Njiru Mbogo alifanya jitihada kubwa kumuepusha na fedheha zaidi.
Mara zote, Mpambe wa Rasi huambatana na bosi wake kwenye gari moja, na huhakikisha kuwa Rais amekaa vizuri na kwa usalama ndani ya gari.
"Na ndio maana wao huwajibika kuwafungulia mlango na kuwafunga mikanda wawapo ndani ya magari, wakati wa misafara," anaeleza Theuri.
Hata hivyo, kulingana na Theuri,majukumu ya Mpambe wa Rais huishia nyumbani kwa kiongozi huyo wa nchi, huku majukumu yote sasa yakihamia kwa walinzi wa Rais, ambao wana mafunzo maalumu ya ulinzi wa viongozi.
Kwa ujumla, ofisi ya Mpambe wa Rais inajukumu la kuratibu shughuli za siku za Rais, ikiwemo kupanga mikutano na ratiba zingine, na kuhakikisha kuwa zinaenda kama zilivyopangwa.
Pia, Mpambe wa Rais anajukumu la kumsaidia kiongozi huyo awape kwenye matukio ya kitaifa ama kimataifa, kama vile kumsaidia kubeba mabegi na wakati mwingine kumhudumia Rais kama vile kummininia maji wakati kiongozi huyo akitoa hutoba.
Hata hivyo, ikitokea hali ambayo itamlazimu Mpambe huyo kutoa msaada wa Rais, basi mtu huyo atawajibika kufanya hivyo kwa wakati ufaao.