Licha ya bunge hilo la EALA kupitisha lugha ya Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha rasmi ya jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mnamo 2021, matumizi yake kwenye mjadala haikuruhusiwa.
Jaribio la Mbunge Dorothe Masirika Nganiza, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, la kutaka kuwasilisha hoja kupitia Kiswahili, lilipingwa vikali na wabunge wenzake walioshikilia kuwa lugha hiyo haikuruhusiwa kutumika kwenye mjadala bungeni kwani kiingereza pekee ndiyo ilifahamika kuwa lugha ya kazi ya EAC
Mbunge wa Sudan Kusini EALA Gabriel Alaak Garang alipinga suala hilo huku akiongeza kuwa iwapo lugha ya Kiswahili ingeruhusiwa, mataifa mengine washirika kama Sudan Kusini nayo yangependekeza lugha ya Kiarabu.
“Mambo yanayohusu bunge la EALA yanafaa kutekelezwa kutumia Kiingereza. Wale wasioweza kujieleza kupitia Kiingereza, wanafaa kutafuta njia zingine mbadala.” alisisitiza.
Spika wa Bunge bwana Joseph Ntakirutimana, ambaye pia ni raia wa Burundi, alisisitiza kuwa sheria na taratibu za Bunge zinaamuru mijadala ifanikishwe kwa Kiingereza, kwani ndio lugha ya kazi bungeni.
Ingawa Kiswahili ni lugha maarufu inayotumika kwa mazungumzo rasmi na mijadala kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, na kupitishwa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, Kiingereza ndio inatambulika kuwa lugha ya kazi.
Hata hivyo Mbunge wa DRC Dorothe alilazimika kutoendelea na maelezo yako kutumia Kiswahili, huku wawakilishi wenzake akiwemo mbunge wa EALA kutoka Sudan Kusini Dkt. Woda Jeremiah Odok Jago na mbunge David Sankok kutoka Kenya, wakitoa wito kwa bunge la EALA kuhakikisha lugha ya Kiswahili imeshirikishwa kuwa lugha ya kazi kwenye bunge hilo.
“Sio eti kuwa wabunge wenzetu kutoka mataifa kama DRC hawawezi kuchangia hoja, lakini changamoto ya lugha ndio tatizo kubwa tunalopaswa kutatua.” Alisema Woda.