Wakaazi wa kambi za muda katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema wanaishi katika hali mbaya baada ya mafuriko kukumba majimbo ya Ituri na Mongala, pamoja na mji mkuu wa Kinshasa, Disemba mwaka jana.
Mafuriko hayo yametokea baada ya mwezi mmoja wa mvua kubwa kunyesha ambayo pia ilisababisha maporomoko ya ardhi na kuporomoka kwa majengo.
Mikoa 18 kati ya 26 ya DRC imeathiriwa kufuatia mvua kubwa ya kipekee katika miezi michache iliyopita, na kuacha zaidi ya watu milioni 2 - karibu asilimia 60 - wanaohitaji msaada, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la UNOCHA.
" Maji ya mafuriko yameripotiwa kuharibu karibu kaya 100,000, shule 1,325, na vituo vya afya 267. Mazao yameharibika katika mashamba yaliyojaa maji, na hivyo kuongeza uwezekano wa uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo," Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto, UNICEF limesema.
Mvua hiyo iliyonyesha ilijaza Mto Congo hadi kiwango chake cha juu zaidi katika zaidi ya miaka 60 na kuwalazimu karibu watu 500,000 kukimbia maji yanayoongezeka.
Mkazi wa moja ya kambi za muda zilizojengwa kwenye uwanja wa kanisa Katoliki viungani mwa mji mkuu, Kinshasa, anasema familia yake inajitahidi kukabiliana nayo.
Nafasi zilizojaa watu
"Takriban mwezi mmoja umepita tangu tuondoke nyumbani kwa sababu ya mafuriko. Tunateseka," alisema Cyprien Seka, ambaye pia ni baba wa watoto watatu.
"Usiku hapa ni wa kutisha. Kuna watu wengi wametapakaa, wamesongamana... tunakosa hewa; huwezi kupumua," amesema mzee wa miaka 55, Pansel Moto Pamba.
Congo ilikuwa na kiwango cha pili cha juu cha miti duniani mnamo 2022, baada ya Brazil, kulingana na Global Forest Watch.