Mazungumzo hayo yalianza wiki iliyopita katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Dar es Salaam, chini ya usimamizi wa IGAD./ Picha : Reuters maktaba 

Waasi kutoka eneo la Oromiya nchini Ethiopia walisema Jumatatu walikuwa nchini Tanzania kwa duru ya pili ya mazungumzo na serikali ya Ethiopia ili kujaribu kumaliza miongo kadhaa ya mapigano.

Mazungumzo hayo yanakuja zaidi ya miezi sita baada ya duru ya kwanza ya majadiliano kati ya Jeshi la Ukombozi wa Oromo (OLA) na serikali ya Ethiopia kumalizika bila makubaliano.

"Tunashikilia azma ya kujitolea kutafuta suluhu la amani la kisiasa," OLA ilisema katika taarifa yake.

Afisa mmoja wa karibu na wasuluhishi hao ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema mazungumzo hayo yalianza wiki iliyopita katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Dar es Salaam, na yanasimamiwa na kundi la kanda ya Afrika la IGAD.

Hata hivyo OLA imesema ilihofia kutangaza mkutano huo mapema kwa kuongopea usalama wa maafisa wake, ambao inadai wamejikuta katik amakabiliano ya hatari.

kwa mujibu wa shirika la Reuters, serikali ya Ethiopia haikutoa jibu la mara moja walipoulizwa.

OLA ni kundi lililoharamishwa la Ukombozi wa Oromo, chama cha upinzani kilichopigwa marufuku hapo awali ambacho kilirejea kutoka uhamishoni baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed - mwenyewe wa kabila la Oromo - kuchukua wadhifa mnamo 2018.

Oromiya, ambayo inazunguka Addis Ababa, mji mkuu, ni nyumbani kwa kabila kubwa zaidi la Oromo nchini Ethiopia na zaidi ya theluthi moja ya watu milioni 110 wa nchi hiyo.

Mzozo katika miaka ya hivi karibuni umesababisha vifo vya mamia ya watu na maelfu ya wengine kuyahama makazi yao katika eneo lenye watu wengi zaidi nchini Ethiopia.

Mazungumzo hayo yanakuja huku kukitokea mapigano kati ya jeshi na kundi la wanamgambo wa Fano katika mji mtakatifu wa Lalibela wiki iliyopita, wakaazi waliambia Reuters. Serikali ilisema eneo hilo lilikuwa na amani.

Reuters