Na Kudra Maliro
Mamlaka nchini DRC zimeazimia kujenga vizimba vya chuma pembezoni mwa Ziwa Edouard kufuatia mfululizo wa matukio ya watu kushambuliwa na mamba katika eneo hilo.
Watu kumi wameuwawa na mamba hao katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, katika maeneo ya Kyavinyonge linalopatikana Kivu Kaskazini.
"Tunazo taarifa za watu 10 kuuwawa na mamba hao kuanzia Novemba 2023. Idadi kubwa ya waliowawa ni wavuvi haramu," Jérémie Tsororo, mwandishi wa habari wa kujitegemea katika eneo la Kyavinyonge ameiambia TRT Afrika.
Kulingana na mwanahabari huyo, tukio la hivi karibuni lilitokea mwisho wa wiki, likimuhusisha mvuvi.
Vizimba vya Chuma
Japokuwa ni ya nadra sana, matukio ya aina hii hutokea wakati wananchi wanapoenda kufua nguo zao au kuteka maji kando ya ziwa hilo.
Msemaji wa ya Taasisi ya Uhifadhi wa Asili ya nchini (ICCN) inayopatikana Kivu ya Kaskazini, amesema kuwa vizimba hivi vitasimikwa kwenye maeneo yanayotembelewa sana na watu ili kuzuia matukio ya aina hiyo.
Ziwa Edouard ni kati ya maziwa makubwa nchini Afrika, likipatikana katika Bonde la Ufa, mpakani mwa DRC (kwa asilimia 71) na Uganda (kwa asilimia 29).
Pia linapatikana ndani ya hifadhi ya Virunga nchini DRC na ile ya Malkia Elizabeth, kwa upande wa Uganda.
Miradi ya Maji
Uvuvi ni shughuli muhimu sana ya kiuchumi inayofanywa na jamii za eneo hilo.
ICCN inapanga kuchimba visima vya maji katika eneo hilo ili kupunguza idadi ya watu wanaokwenda ziwani kutafuta huduma hiyo.
"Hatimaye, ongezeko la mambo katika Ziwa Edouard limewaibua ICCN," amesisitiza Bienvenue Bwende.
Kanuni za uvuvi
Bwende ameendelea kusema," ni kweli kuwa kumekuwa na taarifa za matukio ya watu kuuwawa na kujeruhiwa na mamba katika eneo la Ziwa Edouard, waathirika wengi ni wale wanaojihusisha na uvuvi haramu, hasa kwenye maeneo yasiyo ruhusiwa kufanya shughuli hiyo".
"ICCN imewaasa wavuvi kuheshimu na kuzingatia kanuni zote za uvuvi kwenye Ziwa Edouard, ambazo zitawahakikishia usalama wao," alimalizia Bwende.