Tanzania imejenga vizimba maalumu pembezoni mwa Ziwa Victoria ili kupunguza hatari za watu kushambuliwa na mamba katika eneo la Sengerema, mkoani Mwanza.
Mtafiti huyo wa Mamba kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania, anasema kuwa mpaka sasa, serikali ya Tanzania imejenga vizimba sita, katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema.
Dkt Lipende ameongeza kwa kusema kuwa, matumizi mazuri ya teknolojia ya vizimba hivyo yameonesha ufanisi mkubwa katika kuzuia na kupunguza athari za mashambulio toka kwa mamba ambapo tafiti zilionesha kuwa walishambuliwa zaidi wakati wa kuoga na kufua.
"Wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa kushambuliwa na mamba," Dkt Lipende.
Kulingana na Dkt Lipende, kila kizimba kimoja kina ukubwa wa upana wa mita 30 na urefu wa mita 35 ambapo mita 20 za uzio zipo ndani ya maji na Mita 15 zipo nchi kavu, hivyo kutoa nafasi kwa jamii kutumia eneo hilo kwa uhuru na usalama kwani uzio hutenganisha watu na mamba.
"Pamoja na ujenzi wa vizimba hivi, jamii hazina budi kuwa makini dhidi ya mamba wala watu," amehimiza Dkt Lipende.
Kwa upande wao, wananchi wa eneo hilo wameonesha matumaini yao kwa ubunifu huo katika kuwahakikishia usalama wa kuendelea na shughuli zao za kawaida.
Beatus Maganja, muhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) amesema kuanzia Julai 2023 hadi Mei 2024, mamlaka hiyo iliendesha mikutano 84 ya kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu mbalimbali za kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko katika vijiji 44 na shule 40 ambapo jumla ya watu 53,639 walifikiwa na elimu hiyo
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa mamba na viboko ndio wenye kuhusika kwa kikubwa na migogoro kati ya Wanyamapori na binadamu nchini Tanzania, wakiwa wamesabisha majeraha kwa watu 642.