Na Omar Abdel-Razek
Baadhi ya migogoro inaleta mgawanyika katika dunia, na unaleta madhara makubwa na kuhatarisha usalama wa dunia na uchumi.
Hata hivyo, baadhi ya migogoro husahaulika. Kwa mfano, ule wa Urusi na Ukraine, bila kusahau mgogoro wa Sudan.
Ni takriban miaka miwili sasa, ambapo vita viliibuka nchini Ukraine, mara nyingi vilikuwa vikijulikana kama "vita vya mtu mweupe" kutokana na eneo lake la kijiografia na adui wake, ambae ni Urusi- siku zote akionekana kama tishio la kihistoria kwa Marekani na nchi za Magharibi.
Hii pengine inaweza kuwa sababu ya Marekani kutoa msaada wa dola bilioni 71 kwa Ukraine, huku dola bilioni 43 zilielekwa katika msaada wa kijeshi na usalama. Sehemu nyengine ya dunia nayo ikatoa takriban dola bilioni 50, hayo ni kwa mujibu wa ripoti.
Mgogoro huu, umeifanya Ulaya na Marekani kutathmini uwezo wao wa kijeshi na kuongeza matumizi katika sekta ya ulinzi. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi wa raia 10,000 wamepoteza maisha nchini Ukraine tangu kuanza kwa mapigano mnamo Februari 22, mwaka 2022.
Katika bara la Africa, ambapo kumekuwa na zaidi ya migogoro ya kijeshi 35, mingi inaonekana kama ni midogo katika jukwaa la kimataifa.
Vita vya Sudan, vinaangukia katika nafasi hiyo. Zaidi ya miezi nane tangu kuanza kwake Aprili 2023, tayari vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 12,000. Martin Griffith, mkuu wa Umoja wa Mataifa anaeshughulikia misaada, amesema, vita hivi ni "moja wapo ya majanga makubwa ya kibinadamu kuwahi kutokea katika historia ya hivi karibuni."
Zaidi ya watu milioni 7 wamepoteza makazi, huku kukiwa na zaidi ya 1.5 ambao wanatafuta hifadhi katika nchi jirani.
“Vyombo vya habari”
Jambo la kushangaza, vita vya Sudan havijaleta msukumo wa jumuia ya kimataifa kutafuta suluhu ya kudumu ya kisiasa.
Badala yake, mara nyingi unaonekana kama "mgogoro wa kibinadamu."Sababu moja ya msingi ni mtizamo wa nchi za Magharibi kuhusu migogoro ya Afrika-kimsingi kama migogoro inayosababishwa na makabila kugombania rasilimali.
Msaada wa jumuia ya kimataifa huwa hauonekani kuwa na umuhimu mpaka "migogoro ya kikabila" inapofika hali mbaya. Taarifa za vyombo vya habari kuhusu vita, na 'dunia ya tatu' kwa ujumla, zinatokea tu pale taarifa hizo zinapokuwa na umuhimu wa dunia nyengine.
Hali hii pia ilionekana katika vita vya Somalia baada ya kuanguka kwa utawala wa Siad Barri mwaka 1990. Ulimwengu wa magharibi umebaini kuwa hali ya Somalia ni mbaya pindu tu waharamia wa Kisomali walivyoanza kuwa tishio katika Bahari ya Hindi.
Mtizamo huo unaenda pia kwa viongozi wa mapigano hayo, wanaoitwa 'wakuu wa vita' ambao hamasa yao ni misingi ya kikabila, na maslahi ya kisiasa kama yalivyokubaliwa.
Nchini Sudan, mgogoro ni kati ya Jenerali Abdel-Fattah Burhan, na aliyekuwa msaidizi wake Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu Hamedti.
Hali ya kutoaminiana kati yao, ambao ndio waliofanya mapinduzi ya 2021 dhidi ya utawala wa kiraia, kutofikia makubaliano ya kutawala pamoja, ndio sababu ya kuibuka kwa mgogoro huo.
Mashambulizi ya hivi karibuni ya vikosi vya Hemedti katika eneo la Wad Madani, mji wa tatu kwa ukubwa Sudan, kusini mashariki mwa Khartoum, yameumulika mgogoro huo kwa mara nyengine, ingawa mapigano yanayoendelea Palestina kidogo yamepunguza ufuatiliaji.
Zaidi ya watu 300,000 wamehama makazi yao, wakitafuta hifadhi katika maeneo ya mashariki ya Gedaref, Sennar, na majimbo ya White Nile, hayo ni kwa mujibu ya ripoti ya mashirika ya misaada. Mengi yao, yanaenda kwa mara ya pili baada ya kuondoka Khartoum na vitongoji vyake.
Hali ya jinamizi
Athari za mapigano ya Sudan, zinaweza kuongezeka katika eneo ambalo tayari lina migogoro.
Misri ambayo, ni makazi ya raia wa Sudan zaidi milioni 4 na ina uhusiano wa kihistoria na Sudan, ni miongoni mwa nchi zitakazopata athari kubwa zaidi ya mapigano yanayoendelea nchini Sudan.
Pande zote zinazopigana, zinasukumia lawama kwa mataifa mengine kuhusiana na mgogoro wao.
Mwandishi, Omar Abdel-Razek, alikuwa mhariri BBC Idhaa ya Kiarabu. Anaishi na kufanya kazi London.
Kanusho: Maoni ya mwandishi sio maoni, mtizamo au sera ya habari ya TRT Afrika.