Rambirambi zimeendelea kumiminika kutoka kote duniani kufuatia kifo cha Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima na watu wengine tisa katika ajali ya ndege ya Jumatatu.
Rais Lazarus Chakwera alitangaza kwamba mabaki ya ndege hiyo yamepatikana baada ya utafutaji wa zaidi ya siku moja katika misitu mikubwa na maeneo yenye milima karibu na mji wa kaskazini wa Mzuzu.
Chakwera alisema hakukuwa na walionusurika katika ajali hiyo. Mwili wa makamu wa rais unatarajiwa kusafirishwa kwenda mji mkuu, Lilongwe, baadaye Jumanne.
Rais alipigwa picha akiwa na machozi akiwafariji baadhi ya wanachama wa baraza lake la mawaziri baada ya kutangaza kifo hicho, kulingana na picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Malawi.
Umati waomboleza
Umati umejikusanya katika makao makuu ya chama cha United Transformation Movement (UTM) cha Chilima kuomboleza kiongozi huyo.
Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alisema alihuzunika sana na vifo hivyo.
"Mwenyekiti anatoa rambirambi zake za dhati kwa familia zilizofiwa, na kwa serikali na watu wa Malawi kwa msiba huu mkubwa wa kitaifa," Umoja wa Afrika ulisema.
Waziri Mkuu wa Iceland Bjarni Benediktsson alisema ilikuwa heshima kutumia muda na Chilima wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Malawi.
"Niliathiriwa sana na maono yake na upole wake. Mawazo yangu yako na familia yake na wote walioguswa," alisema katika chapisho kwenye jukwaa la X.
'Wakati wa janga'
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alielezea ajali hiyo ya ndege kama "wakati wa janga".
"Huu ni msiba uliogusa nchi yetu na kanda yetu na tunawaombea watu wa Malawi wabarikiwe na nguvu na amani zinazohitajika katika kipindi hiki cha huzuni kubwa na maombolezo ya kitaifa," alisema katika taarifa.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu alisema alipokea habari hizo kwa huzuni kubwa.
"Natoa pole zetu za dhati kwa Rais Lazarus Chakwera, watu wa Jamhuri ya Malawi, familia na marafiki," alisema.
'Inasikitisha sana'
Rais wa Nigeria Bola Tinubu alielezea ajali hiyo ya ndege kama "tukio linalosikitisha sana".
"Rais anahakikisha taifa la Malawi msaada wa Nigeria wakati huu wa maombolezo," ofisi yake ilisema.
Rais wa Zambia Hakainde Hichilema alitoa "rambirambi zake za dhati" kwa watu wa Malawi.
"Tunaomba Mungu awape nguvu na faraja wakati huu mgumu. Zambia inaomboleza nanyi," alisema.
Rais wa zamani wa Malawi Joyce Banda alisema alihuzunishwa na kifo cha makamu wa rais.
"Huu ni wakati mgumu kwa nchi," alisema.