Ndege ya Safarilink ya Dash 8 ilikuwa na abiria 39 n awahudumu 5 / Picha : TRT Afrika

Ndege mbili zimegongana angani jijini Nairobi muda mfupi baada ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Wilson Jumanne asubuhi.

Mamlaka ya usafiri wa anga nchini Kenya KCAA imethibitisha katika taarifa kwenye mtandao wa X kuwa ndege aina ya Dash 8 kutoka kampuni ya Safarilink imegongana angani na ndege ndogo ya wanafunzi aina ya Cessna 172 mwendo wa saa tatu na robo asubuhi.

Hakuna maelezo kamili juu ya majeruhi au vifo vyovyote kutoka kwa vyombo husika.

Ndege ya Safarilink ilikuwa safarini kuelekea Diani, pwani ya Kenya ikiwa na abiria 39 na wahudumu watano huku ndege ya mafunzo ya Cessna 172 inamilikiwa na chuo cha mafunzo ya urubani ya Ninety-Nines.

Mamlaka ya KCAA imesema kuwa uchunguzi umeanzishwa unaohusisha vyombo mbali mbali husika, ukiongozwa na idara ya ajali za ndege nchini Kenya AAID, kujua chanzo cha ajali hiyo.

Awali kampuni ya Safarilink ilichapisha taarifa katika mtandao wake wa X, zamani Twitter kuwa ndege yao moja imelazimika kutua ghafla baada ya mlio mkubwa kusikika, japo hawakutaja iwapo ilikuwa kugongana au mlipuko mwingine.

Walioshuhudia wanasema ndege hiyo ya mafunzo ilianguka katika hifadhi ya wanyama ya Nairobi, iliyo karibu na uwanja wa ndege wa Wilson.

TRT Afrika