Jeshi la Malawi linaendelea kuitafuta ndege iliyombeba Makamu wa Rais wa nchi hiyo Saulos Klaus Chilima na wengine tisa.
Chilima alikuwa ameambatana na mke wa zamani wa Rais wa nchi hiyo Bakili Muluzi, Shanil Dzimbiri, safarini kuelekea kwenye mazishi ya waziri wa zamani wa Malawi, kabla haijapoteza mawasiliano na rada.
Ndege hiyo iliruka kutoka uwanja wa ndege wa mjini Lilongwe saa tatu asubuhi na ilitarajiwa kutua ndani ya dakika 45.
Chilima ni nani?
Mtaalamu huyo wa uchumi alizaliwa Februari 12, 1973 katika wilaya ya Ntcheu iliyo katikati ya Malawi.
Chilima alipata shahada ya Uzamivu katika Usimamizi wa Maarifa kutoka Chuo Kikuu cha Bolton nchini Uingereza.
Kabla ya kuingia katika siasa, Chilima alianzia kwenye sekta binafsi na kushika nafasi za juu katika kampuni mbali mbali zikiwemo Airtel Malawi na Unilever.
Chilima alimuoa Mary Chilima, aliyekuwa mfanyakazi wa benki, na ni baba wa watoto wawili.
Chilima aliingia rasmi kwenye siasa akiwa mgombea mwenza wa Peter Mutharika katika uchaguzi wa urais wa 2014, ambapo walishinda na akachaguliwa kama Makamu wa Rais.
Alisifika sana kwa mageuzi yake ya kiuchumi katika nchi hiyo, ikiwemo kupambana na ufisadi.
Mwaka 2018, alianzisha Umoja wa Mageuzi (UTM) baada ya kutofautiana na Rais Mutharika na Chama cha Maendeleo cha Kidemokrasia (DPP). Aligombea urais katika uchaguzi wa 2019 lakini hakushinda.
Hata hivyo, katika marudio ya uchaguzi wa urais wa 2020, alichaguliwa tena kuwa Makamu wa Rais baada ya kupita kama mgombea mwenza wa Rais wa sasa, Lazarus Chakwera.
Hata hivyo, Chilima aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Mpango na Uchumi akiwa anasifika kwa kuchochea mabadiliko makubwa katika sekta ya umma.
Kushirikiana katika utafutaji
Wakati huohuo, Waziri wa habari wa Malawi Moses Kunkuyu amesema kuwa Mamlaka ya Mawasiliano ya nchi hiyo (Macra) inashirikiana na mamlaka za mawasiliano za Tanzania na Zambia katika kutafuta ndege hiyo.
Hii si mara ya kwanza kwa ndege na helikopta za viongozi kupotea na kisha kuripotiwa kupata ajali.
Mwezi uliopita, helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Iran Ebrahim Raisi ilianguka na kufuatia hali mbaya ya hewa. Kiongozi huyo pamoja na ujumve wake walipoteza maisha katika tukio hilo.
Mwezi Aprili mwaka huu, Mkuu wa Majeshi wa Kenya Jenerali Francis Ogolla alipoteza maisha baada ya helikopta waliyokuwa wanasafiria kuanguka katika eneo la Elgeyo-Marakwet