Idadi ya waliofariki kutokana na Kimbunga Freddy Kusini Mashariki mwa Afrika imepanda hadi 569, kulingana na takwimu za hivi punde za majeruhi.
Nchini Malawi, vifo sasa vimefikia 476, huku watu 918 zaidi wakiwa wamejeruhiwa na takribani 349 hawajulikani walipo, shirika la kudhibiti majanga limesema.
Zaidi ya watu 490,000 waliokimbia makazi kwa sasa wanahifadhiwa katika kambi 533, shirika hilo liliongeza.
Katika nchi jirani ya Msumbiji, takriban watu 76 wamefariki na wengine 34 kujeruhiwa, kulingana na ripoti ya Taasisi ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa.
Kimbunga hicho kimeathiri watu 540,563 na kuharibu nyumba 33,292.
Baadhi ya shule 892 na vituo 80 vya huduma za afya pia viliathirika, na zaidi ya kilomita 5,000 za miundombinu ya barabara imeathiriwa, iliongeza.
Zaidi ya watu 64,400 wanaishi katika vituo vya malazi vinavyo endeshwa na serikali katika majimbo sita.
Takriban watu 17 waliuawa katika kisiwa cha Madagascar wakati kimbunga hicho kilipotua kwa mara ya kwanza Februari 21.
Mamlaka katika nchi zote tatu zinatarajia idadi ya waliofariki kuongezeka katika siku zijazo huku shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea katika maeneo kadhaa yaliyoathiriwa.