Ndege

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Sasa ni rasmi.

Saulos Chilima, Makamu wa Rais wa Malawi amefariki dunia kufuatia ajali ya ndege iliyotokea Juni 10, 2024.

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ametangaza kuwa makamu wake Dkt Saulos Klaus Chilima na wengine tisa wamefariki dunia baada ya ndege waliyokuwa wanasafiria kuanguka katika msitu wa Chikangawa katika eneo la Mzimba, nchini Malawi, Juni 10, 2024.

Chilima, na wengine tisa walikuwa wameabiri ndege ya Jeshi la Ulinzi la Malawi (MDF) iliyoripotiwa kutoweka kwenye mawasiliano ya rada mara baada ya kushindwa kutua kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mzuzu siku ya Jumatatu.

Ndege hiyo iliruku kutoka uwanja wa ndege wa Mzuzu saa moja na dakika tano asubuhi ya Jumatatu na kutua katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu mjini Lilongwe, kisha ikamchukua Makamu wa Rais, tayari kurudi Mzuzu.

Ndege iliyokuwa imembeba Chilima na abiria wengine tisa./Picha: Wengine

Ndege hiyo pia ilikuwa imembeba Shanil Muluzi, mke wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Bakili Muluzi . Walikuwa wanaenda katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Sheria Ralph Kasambara aliyefariki siku ya Ijumaa.

Chilima ni nani?

Mtaalamu huyo wa uchumi alizaliwa Februari 12, 1973 Chilima alipata shahada ya Uzamivu katika Usimamizi wa Maarifa kutoka Chuo Kikuu cha Bolton nchini Uingereza.

Kabla ya kuingia katika siasa, Chilima alianzia kwenye sekta binafsi na kushika nafasi za juu katika kampuni mbali mbali yakiwemo Airtel Malawi na Unilever.

Aliingia rasmi kwenye siasa akiwa mgombea mwenza wa Peter Mutharika katika uchaguzi wa urais wa 2014, ambapo walishinda na akachaguliwa kuwa Makamu wa Rais.

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima(kulia) akiwa na Rais wa nchi hiyo Lazarus Chakwera./Picha: Wengine

Chilima alijizolea sifa kutokana na mageuzi yake ya kiuchumi katika nchi hiyo, ikiwemo kupambana na ufisadi.

Mwaka 2018, alianzisha Umoja wa Mageuzi (UTM) baada ya kutofautiana na Rais Mutharika na Chama cha Maendeleo cha Kidemokrasia (DPP).

Aligombea urais katika uchaguzi wa 2019 lakini hakushinda.

Hata hivyo, katika marudio ya uchaguzi wa urais wa 2020, alichaguliwa tena kuwa Makamu wa Rais baada ya kupita kama mgombea mwenza wa Rais wa sasa, Lazarus Chakwera.

Ajali za anga hivi karibuni

Hii si mara ya kwanza kwa ndege na helikopta za viongozi kupotea na kisha kuripotiwa kupata ajali.

Mwezi uliopita, helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Iran Ebrahim Raisi ilianguka kufuatia hali mbaya ya hewa. Kiongozi huyo alipoteza maisha akiwa na ujumbe wake.

Mwezi Aprili mwaka huu, Mkuu wa Majeshi wa Kenya Jenerali Francis Ogolla alipoteza maisha baada ya helikopta waliyokuwa wanasafiria kuanguka katika eneo la Elgeyo-Marakwet.

TRT Afrika